OLE Gunnar Solskjaer, Kocha Mkuu wa Manchester United amesema kuwa kichapo cha mabao 5-0 mbele ya Liverpool ni moja ya siku nyeusi kwake katika kazi ya kuwaongoza mastaa wa Manchester United.
Ikiwa Uwanja wa Old Trafford katika mchezo wa Ligi Kuu England ilishuhudia vijana wa Kocha Mkuu Jurgen Klopp wakiwatungua mabao matano kupitia kwa Naby Keita dakika ya 5,Diogo Jota dakika ya 13,huku Mohamed Salah akifunga hat trick dakika ya 38,45 na 50.
Kipigo hicho pia kimeibua maswali kuhusu safu ya ulinzi ya Manchester United licha ya kuwa imetumia gharama kubwa kuwa na nyota hao ikiwa ni pamoja na Harry Maguire ambaye hakuwa na chaguo wakati timu hiyo ikitunguliwa mabao hayo huku kiungo Paul Pogba akionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 60 baada ya kumchezea faulo Naby.
Pia mshambuliaji wao tegemeo Cristiano Ronaldo alikwama kuipa ushindi timu hiyo akiwa pamoja na mshikaji wake Bruno Fernandes ambao walikuwa wakipewa nafasi kuibeba timu hiyo kwenye upande wa kucheka na nyavu.
Solskjaer amesema kuwa sio jambo jepesi kwake kusema jambo lolote lakini anaamini kwamba kichapo hicho ni giza kubwa kwake na hawakuwa imara katika kutumia nafasi ambazo walizipata mbele ya Liverpool.