WASHIKA BUNDUKI WAKIWASHA HUKO LIGI KUU ENGLAND

BUNDUKI za washika bunduki Klabu ya Arsenal ziliweza kujibu kwa furaha baada ya kuwatungua Aston Villa katika mchezo wa Ligi Kuu England mabao 3-1 na kuwafanya waweze kusepa na pointi tatu mazima.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Emirates vijana wa Kocha Mkuu, Mikel Arteta walitawala kila idara huku mabao yao yakipachikwa na Thomas Partey dakika ya 23,Pierre Aubameyang dakika ya 45 na Emile Smith Rowe dakika ya 56.

Kwa upande wa Aston Villa yenye pointi 10 baada ya kucheza mechi 9 ikiwa nafasi ya 13 bao lao lilifungwa na Jacob Ramsey ilikuwa dakika ya 82 likawafuta machozi vijana hao ila pointi walikosa mazima.

Ni mashuti 22 yalipigwa na Arsenal yenye pointi 14 ikiwa nafasi ya 9 baada ya kucheza mechi 9 na kushinda mechi nne ambapo katika mashuti hayo ni mashuti 9 yalilenga lango huku wapinzani wao Aston Villa wao walipiga mashuti 10 na mashuti manne pekee yalilenga lango katika mchezo huo wa Ligi Kuu England.

Partey aliweza kufunga bao lake la kwanza ndani ya Arsenal huku Arsenal ikiaminika kwamba inaanza kurudi kwenye ubora wake taratibu kwa kuwa haikuanza mwendo wa msimu wa 2021/22 vizuri.