Mamlaka za Marekani zimeunda kikosi kazi maalum (task force) kitakachosimamia usalama na uchunguzi mkali wa mashabiki, wachezaji na wageni wote watakaofika nchini Marekani wakati wa Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Hatua hiyo imekuja baada ya matukio kadhaa ya kuhojiwa na kucheleweshwa kwa watu wanaohusiana na michuano hiyo, ikiwemo mshambuliaji wa Iraq Aymen Hussein aliyekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa O’Hare, Chicago, na kuhojiwa kwa saa saba kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini kwa ajili ya mechi ya kirafiki.
Hata hivyo, mpiga picha wa timu ya taifa ya Iraq, Talal Salah, alizuiliwa kuingia Marekani baada ya kuhojiwa kwa saa 10, hatua iliyozua mjadala mkubwa kuhusu mchakato wa vibali na ulinzi wa mipaka.
Mamlaka ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani (U.S. Customs and Border Protection) imesema imeanzisha “CBP World Cup Task Force” ili kuratibu usalama katika miji yote itakayohost Kombe la Dunia, pamoja na kuongeza wataalamu na mifumo ya ukaguzi.
CBP imesema pia itahakikisha usalama wa viwanja, kudhibiti bidhaa bandia, pamoja na kuweka maeneo yasiyoruhusiwa kuruka ndege (no-fly zones) karibu na viwanja vya mashindano.
Hata hivyo, baadhi ya Wamarekani wenye asili ya Kiarabu wameikosoa hatua hiyo, wakisema inazua maswali kuhusu usawa wa mchakato wa visa na ukaguzi wa wageni, hasa baada ya baadhi ya watu kuonekana wakizuiliwa licha ya kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na timu zao.