Real Madrid imeripotiwa kuwatoza faini ya euro 500,000 kila mmoja viungo wake Federico Valverde na Aurélien Tchouaméni kufuatia kuhusishwa katika mzozo uliotokea wakati wa mazoezi ya timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, wawili hao waliingia kwenye mabishano makali wakati wa mazoezi yenye ushindani mkubwa, kabla hali hiyo haijageuka kuwa ya vurugu na kuwalazimu makocha pamoja na baadhi ya wachezaji kuingilia kati ili kutuliza mazingira ndani ya kikosi.
Inaelezwa kuwa uongozi wa Madrid haukufurahishwa na tukio hilo, hasa ikizingatiwa kuwa timu ipo katika kipindi muhimu cha kumalizia msimu wa La Liga na inapigania mafanikio kwenye michezo iliyobaki.
Kutokana na hali hiyo, klabu hiyo imechukua hatua za kinidhamu kwa lengo la kulinda nidhamu, mshikamano na utulivu wa kikosi.
Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa Valverde na Tchouaméni tayari wamezungumza na kuweka tofauti zao pembeni kwa maslahi ya timu.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani, huku baadhi wakihusisha mvutano huo na presha kubwa ya ushindani ndani ya kikosi cha Real Madrid.