Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, ametetea uamuzi wa kuanzishwa kwa mapumziko ya lazima ya maji (hydration breaks) katika Kombe la Dunia 2026, akisisitiza kuwa uamuzi huo hauhusiani na maslahi ya kibiashara bali ni kwa sababu za kiusalama na kiutendaji kwa wachezaji.
Kwa mujibu wa mfumo huo mpya, kila mchezo unasimama kwa dakika tatu katika dakika ya 22 na 67 ili kuruhusu wachezaji kupata maji na pia makocha kutoa maelekezo ya kiufundi uwanjani.
Hatua hiyo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa makocha, wachezaji na mashabiki, baadhi wakilalamika kuwa mapumziko hayo yanavunja mwelekeo wa mchezo na kubadilisha uhalisia wa soka la ushindani wa kawaida.
Wakosoaji akiwemo kocha wa timu ya taifa ya England Thomas Tuchel na kocha wa Uruguay Marcelo Bielsa wamesema mapumziko hayo yanaathiri mtiririko wa mchezo na kupunguza kasi ya ushindani uwanjani.
Hata hivyo, Infantino amesisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha usawa wa mazingira kwa timu zote, hasa kutokana na hali ya joto inayopatikana katika viwanja mbalimbali vya Amerika Kaskazini vinavyotumika kwenye michuano hiyo.
Ameongeza kuwa mabadiliko hayo pia yanalenga kulinda afya ya wachezaji, hasa kutokana na ratiba ngumu ya mashindano ambapo timu zinaweza kucheza mechi nyingi ndani ya siku chache.
Baadhi ya makocha na wachezaji akiwemo Virgil van Dijk na kocha wa Spain Luis de la Fuente wameunga mkono nia ya kulinda afya za wachezaji, ingawa wamehoji umuhimu wa mapumziko hayo katika viwanja vyenye hali ya hewa ya kawaida au vilivyo funikwa.
FIFA imesisitiza kuwa mapumziko hayo hayapunguzi ushindani wa mchezo, bali yanasaidia wachezaji kudumisha kiwango cha juu cha uchezaji katika mechi nzima.