TIMU SITA ZENYE SAFU KALI YA USHAMBULIAJI BONGO

WAKATI mwingine tena umefika ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kufungua zawadi kwa ndugu jamaa na marafiki kwa lugha ya kigeni ni Happy Boxing Day kwenye anga za michezo kuna wale waliotoa zawadi mapema kwa kufunga mabao mengi.

Hapa tunakuletea timu sita ambazo zinasafu kali kwenye upande wa ushambuliaji namna hii:-

Azam FC mabao 35

Kwenye namba moja wametulia kwa 2023 wakiwa na uhakika wa kuanza 2024 wakiwa hapo kwa kuwa hakuna atakayewashusha kwa sasa ni Azam FC wakiwa na pointi zao 31.

Kipre Junior ni namba moja kwenye kutengeneza pasi za mabao akiwa nazo 6 na timu hiyo ina jumla ya mabao 35 ikiwa namba moja kwenye safu kali zenye mabao mengi ndani ya Bongo.

Kinara wa mabao ni Feisal Salum mwenye mabao 8 pia katengeneza pasi nne za mabao hivyo kahusika kwenye mabao 12.

Yanga mabao 31

Wametulia namba mbili kwenye ligi wakiwa na safu namba mbili kwenye utupiaji wa mabao. Kinara wa mabao ni Aziz KI mwenye mabao 10 kama ilivyo namba ya jezi yake mgongoni kwa kiungo huyu.

Namba moja kwa kutengeneza pasi za mwisho ni beki wa kupanda na kushuka Kouassi Yao mwenye pasi tano kibindoni ana bao moja kibindoni. Kahusika kwenye mabao matano kati ya 31.

Simba mabao 23

Wapo namba tatu kwenye msimamo hata kwenye upande wa kutupia mabao ipo hapohapo namba tatu. Mkali wao wa kucheka na nyavu ni Jean Baleke mwenye mabao 8.

Mkali wa kutengeneza pasi za mwisho ni Luis Miquissone na Mohamed Hussein Zimbwe Jr hawa wote wana pasi tatutatu za mabao.

Singida Fountain Gate mabao 17

Ni namba tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa ni namba nne katika safu yenye ukali wa kutupia ikiwa na mabao 17. Mkali wao wa kucheka na nyavu ni Marouf Tchakei akiwa katupia mabao matano kibindoni.

KMC mabao 15

Ipo nafasi ya nne kwenye msimamo na kwa upande wa utupiaji ni namba tano. Mkali wa kucheka na nyavu ni Wazir Junior akiwa katupia mabao 7 kibindoni.

Mtambo wao wa mabao ni Awesu Awesu ana pasi nne za mabao. Kibindoni ina jumla ya pointi 21 baada ya kucheza mechi 14.

Mtibwa Sugar mabao 14

Ajabu na kweli ikiwa ni maana halisi ya mpira dakika 90. Kwenye ligi inafunga 2023 ikiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo. Pointi zake kibindoni ni pointi 8. Ilishinda mechi mbili kati ya 14 ambazo ilicheza.

Ina wastani wa kufunga bao moja kwenye kila dakika 90 hivyo huenda safu ya ulinzi ikiongeza umakini kutakuwa na mwendo wa kipekee ndani ya 2024 katika kuukamilisha msimu wa 2023/24.

Ni mabao 29 safu ya ulinzi iliokota kwenye mechi 14 ikiwa ni namba moja kwa timu iliyoruhusu mabao mengi ndani ya ligi kwa 2023. Mabox yake kwenye upande wa ulinzi yalitobolewa.