Utani Wa Mbappé Wazua Dhoruba China, Wadhamini Wamgeukia!

Nyota wa soka wa Ufaransa na klabu ya Real Madrid, Kylian Mbappé, amejikuta katikati ya mjadala mkubwa nchini China baada ya kauli yake ya utani kuhusu picha ya mtandaoni inayomfananisha na aliyekuwa kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong, kuzua hasira kwenye mitandao ya kijamii.

Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa nchini China huku baadhi ya kampuni zilizokuwa zikishirikiana kibiashara na mchezaji huyo zikianza kuvunja mikataba naye, wakati Shirika la Habari la China (China Media Group), linalomiliki kituo cha televisheni cha CCTV, likisitisha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).

Mzozo huo ulianza baada ya kipande cha mahojiano ya Mbappé kusambaa mtandaoni, ambapo alizungumzia picha ya mzaha inayoweka sura yake kwenye mwili wa mtu anayefanana na Mao Zedong, kiongozi aliyeongoza mapinduzi ya Kikomunisti nchini China na kuanzisha Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949.

Ingawa Mbappé hakumtaja Mao kwa jina katika mahojiano hayo, utani huo ulitafsiriwa na baadhi ya Wachina kama kitendo cha kumdhalilisha mtu anayeheshimiwa sana katika historia ya nchi hiyo.

Kutokana na shinikizo hilo, Mbappé alitoa kauli ya kuomba radhi akisema anajutia maoni yake ambayo hayakuwa na busara. Klabu yake ya Real Madrid pamoja na La Liga nazo zilitoa ujumbe wa kuomba radhi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alieleza kuwa maneno na vitendo vinavyoumiza hisia za wananchi wa China vitakabiliwa na upinzani kutoka sehemu mbalimbali za jamii ya nchi hiyo.

Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba licha ya hasira kubwa iliyojitokeza kwenye mitandao ya kijamii, Wachina wengi hawakufahamu kikamilifu maneno yaliyotamkwa na Mbappé. Mfumo mkali wa udhibiti wa maudhui kwenye intaneti nchini humo ulifanya iwe vigumu kwa watumiaji wengi kupata maelezo ya moja kwa moja kuhusu chanzo cha mzozo huo.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walijaribu kuelezea tukio hilo kwa kutumia mafumbo kama vile kumrejelea Mao kama mtu anayepatikana kwenye noti ya yuan 100 au kumuita ‘mwalimu’, badala ya kumtaja moja kwa moja.

Mao Zedong alifariki mwaka 1976, lakini bado ana nafasi kubwa katika historia na siasa za China. Utawala wake ulihusishwa na matukio makubwa ya kihistoria, yakiwemo kampeni ya Great Leap Forward na Mapinduzi ya Utamaduni, yaliyosababisha vifo vya mamilioni ya watu na misukosuko mikubwa katika jamii ya China.

Kwa upande mwingine, baadhi ya Wachina wanaoishi nje ya nchi walikuwa na mtazamo tofauti, wakionyesha kumuunga mkono Mbappé na kukosoa hatua za udhibiti wa maoni zinazohusishwa na mamlaka za China.

Aidha, kampuni ya bidhaa za maziwa ya Mengniu, ambayo ni mmoja wa wadhamini rasmi wa Kombe la Dunia la FIFA, ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizokatisha ushirikiano wa kibiashara na nyota huyo kufuatia mzozo huo.

Hadi sasa, China Media Group haikuwa imetangaza rasmi kurejesha matangazo ya La Liga, huku akaunti ya Mbappé kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo ikiwekewa zuio la watumiaji wapya kumfuata.

Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu mipaka ya utani, uhuru wa kujieleza, heshima kwa viongozi wa kihistoria na namna mitazamo ya kisiasa inavyoweza kuathiri biashara na michezo ya kimataifa.