Aliyekuwa nahodha na nyota wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, ametoa wito mzito kwa familia ya Glazer kuiuza klabu hiyo haraka iwezekanavyo, akieleza kuwa muda wao wa kuendelea kuiongoza timu hiyo umefika mwisho.
Neville alitoa kauli hiyo kupitia kipindi cha _Stick To Football_, akionyesha kutoridhishwa na namna familia ya Glazer inavyoisimamia klabu hiyo, hasa kutokana na mzigo mkubwa wa madeni, changamoto za miundombinu na kukosekana kwa mafanikio ya kudumu ndani ya uwanja.
“Inabidi wauze timu sasa hivi. Kwa sasa hatuna cha kusubiri, mwisho wao umefika. Kuna deni la pauni bilioni 1.2 hapo Manchester United. Klabu imefungwa mikono kwa njia nyingi sana,” alisema Neville.
Nyota huyo wa zamani alieleza kuwa licha ya Manchester United kutumia takribani pauni bilioni 1.4 katika usajili wa wachezaji ndani ya kipindi cha miaka 15 iliyopita, matumizi hayo hayajaisaidia klabu kurejea katika ubora wake wa zamani, huku madeni yakiendelea kuwa sehemu ya changamoto kubwa zinazoikabili.
Alisisitiza kuwa hali ya kifedha ya klabu inatia wasiwasi, akidai bado kuna madeni makubwa yanayohusiana na usajili wa wachezaji pamoja na madeni mengine ya kifedha.
Neville pia alikosoa namna familia ya Glazer inavyoonekana kuwa mbali na maisha ya kila siku ya klabu hiyo, huku ikiendesha shughuli zake nchini Marekani, hasa Tampa, Florida.
Kwa mujibu wa Neville, Manchester United imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo hali ya uwanja wa Old Trafford unaohitaji maboresho makubwa, huku kukiwa na mipango ya kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya.
Aidha, aligusia kipindi kirefu cha kukosekana kwa mafanikio makubwa tangu kuondoka kwa kocha Sir Alex Ferguson mwaka 2013, akieleza kuwa miaka 13 hadi 14 iliyopita imekuwa migumu kwa klabu hiyo kurejesha hadhi yake ya ushindani.
Kwa mtazamo wa Neville, familia ya Glazer imekuwa na muda wa kutosha kuiongoza Manchester United, lakini sasa ni wakati wa kuachia nafasi kwa wamiliki wapya wenye maono na dhamira ya kuirejesha klabu hiyo katika kilele cha soka la dunia.
Kauli hiyo imeibua tena mjadala kuhusu mustakabali wa Manchester United na iwapo mabadiliko ya umiliki ndiyo yatakuwa hatua muhimu ya kuirejesha klabu hiyo kwenye mafanikio ambayo mashabiki wake wamekuwa wakiyatarajia kwa muda mrefu.