Nyota wa soka kutoka Ureno, Cristiano Ronaldo, amezidi kusogea karibu na kufikisha mabao 1,000 katika maisha yake ya soka baada ya kufunga hat-trick na kuisaidia klabu yake ya Al-Nassr kuibuka na ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Al-Kholood katika mchezo wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, alifunga mabao matatu ndani ya dakika 15 za kipindi cha pili, na kufikisha jumla ya mabao 985 katika maisha yake ya soka.
Katika mchezo huo, Al-Nassr ilipata ushindani mkali baada ya timu hizo kufungana mabao 2-2, kufuatia mabao ya Angelo Gabriel na Sadio Mané kwa upande wa Al-Nassr. Hata hivyo, Ronaldo aliamua matokeo kwa kufunga mabao matatu yaliyoiwezesha timu yake kupata ushindi.
Mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ureno, João Félix, alikuwa miongoni mwa waliochangia ushindi huo kwa kutoa pasi nne za mabao, zikiwemo mbili zilizozaa mabao ya Ronaldo.
Hat-trick hiyo imekuwa ya 67 kwa Ronaldo katika maisha yake ya soka. Kati ya hizo, amefunga hat-trick saba akiwa Al-Nassr, 44 Real Madrid, 10 timu ya taifa ya Ureno, tatu Manchester United na tatu Juventus.
Kwa sasa, Ronaldo anahitaji mabao 15 pekee kufikisha idadi ya kihistoria ya mabao 1,000, hatua ambayo itakuwa miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi katika historia ya soka.
Ronaldo, ambaye amewahi kutwaa mataji ya ligi nchini England, Hispania, Italia na Saudi Arabia, pia ndiye mfungaji bora wa muda wote katika historia ya soka la timu za taifa za wanaume.
Akiwa ameitumikia Al-Nassr kwa karibu miaka minne, Ronaldo amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na klabu hiyo.
Kwa upande wa msimamo wa ligi, Al-Nassr inashika nafasi ya pili ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya vinara Al-Qadsiah.
**Je, Ronaldo ataweza kufikisha mabao 1,000 kabla ya kutundika daruga? Dunia ya soka inasubiri kwa hamu kuona historia hiyo ikiandikwa