Timu za Tanzania zimeanza kwa matokeo mazuri katika mashindano ya klabu Afrika, huku Simba SC na Singida Black Stars zikirejea nyumbani na ushindi katika mechi zao za kwanza za raundi ya kwanza ya kufuzu.
Simba SC ilianza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) 2026/27 kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Bingu National Stadium nchini Malawi.
Bao pekee la Simba lilifungwa dakika ya 65 na Oura, huku kipa Djibril Kassim akihusishwa na assist ya bao hilo.
Kwa upande mwingine, Singida Black Stars ilitoa onyesho kali zaidi baada ya kuichapa Al-Ghazala SC Wau ya Sudan Kusini kwa mabao 7-1 ugenini katika raundi ya kwanza ya kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Tegisi alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga hat-trick ndani ya kipindi cha kwanza, akifunga dakika za 20, 23 na 32.
Sheikhan aliongeza bao la nne dakika ya 41, kabla ya Sowah kufunga dakika ya 63. Henry alifunga bao la sita dakika ya 86, huku Sowah akifunga tena dakika ya 90 kukamilisha ushindi mkubwa wa Singida.
Matokeo hayo yamewapa Simba na Singida mwanzo mzuri katika safari zao za kuwania nafasi ya kufuzu hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika.