Kapombe, Kibabage Waachwa Dar, Simba Yakwea Pipa Kwenda Malawi

NAHODHA wa Simba SC, Shomari Kapombe, ni miongoni mwa wachezaji walioachwa Dar es Salaam wakati kikosi cha timu hiyo kikikwea pipa kuelekea Malawi kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mighty Wanderers.

Simba SC, inayofundishwa na Kocha Mkuu Steve Barker, ina kibarua cha kusaka ushindi katika mchezo huo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, unaotarajiwa kuchezwa Septemba 6, 2026 saa 9:00 alasiri.

Msafara wa Simba uliondoka leo, Septemba 4, 2026, ukiwa na jumla ya wachezaji 22 waliofanyiwa mchujo na benchi la ufundi.

Miongoni mwa wachezaji waliokwea pipa kuelekea Malawi ni Clatous Chama, Libasse Gueye, Ibrahim Doumbia, Ellie Mpanzu, Rushine, Hussen Abel, Duchu na Yusuph Kagoma.

Akizungumza kuhusu wachezaji walioachwa Dar es Salaam, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema sababu za kutosafiri kwao zinatofautiana, zikiwemo majeraha na maamuzi ya kiufundi.

“Wachezaji ambao wanabaki kutokana na majeruhi ni nahodha Shomari Kapombe, Nickson Kibabage, Hamza Jr, Wilson Nangu na Yakoub Suleman, hawa bado wanaendelea na matibabu,” amesema Ahmed Ally.

Ameongeza kuwa wachezaji wengine wamebaki Dar es Salaam kutokana na sababu za kiufundi.

“Wachezaji ambao wanabaki kutokana na sababu za kiufundi ni Kelvin Nashon, Daud Semfuko na Ibrahim Nindi,” amesema.

Simba sasa inaelekeza nguvu zake katika mchezo huo wa hatua ya awali, huku kikosi kilichosafiri kikitarajiwa kuanza kibarua cha kuwania matokeo mazuri ugenini dhidi ya Mighty Wanderers.