Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ameomba radhi kufuatia dosari zilizojitokeza katika mchakato wa kuwasilisha pendekezo la kuruhusu wawekezaji binafsi kuwekeza katika baadhi ya mashindano ya shirikisho hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa FIFA kukiri kuwa kulikuwa na mapungufu ya kiutaratibu, hususan kutoshirikishwa ipasavyo kwa Baraza la FIFA na vyama wanachama kabla ya mpango huo kuwasilishwa rasmi.
Infantino, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafström, alituma barua ya kuomba radhi kwa makamu wa marais wa FIFA, Baraza la FIFA pamoja na vyama wanachama 211, akiahidi kuwa taratibu za maamuzi zitaboreshwa ili kuepusha makosa kama hayo siku zijazo.
Licha ya kuomba radhi, Bodi ya Menejimenti ya FIFA imesisitiza kuwa bado ina imani kamili na Infantino na itaendelea kumuunga mkono katika kuongoza shirikisho hilo.
Pendekezo lililozua mjadala lilihusu kuanzishwa kwa kampuni mpya iitwayo FIFA Forward Enterprise (FFE), ambayo ingefungua nafasi kwa sekta binafsi kuwekeza katika mashindano makubwa ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia la Wanaume na la Wanawake.
Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) lilikuwa miongoni mwa wakosoaji wakuu wa mpango huo, likidai kuwa uliandaliwa na kuwasilishwa bila uwazi wa kutosha, jambo lililozua maswali kuhusu utawala ndani ya FIFA.
Wakati huohuo, FIFA imekanusha madai kwamba Infantino aliiahidi Morocco kuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Dunia 2030 ili kupata uungwaji mkono wa pendekezo hilo. Shirikisho hilo limesema taarifa hizo si za kweli na kusisitiza kuwa uamuzi kuhusu uwanja utakaotumika kwa mchezo wa fainali bado haujafanyika.