LONDON: Klabu ya Arsenal imeendelea na mazungumzo na Newcastle United kuhusu uhamisho wa kiungo nyota wa Brazil, Bruno Guimaraes, huku kukiwa na matumaini kwamba pande hizo mbili zinaweza kufikia makubaliano.
Taarifa kutoka Sky Sports News zinaeleza kuwa kuna matumaini ya tahadhari kuwa dili hilo linaweza kukamilika, huku Guimaraes akisubiri ruhusa ya kusafiri kwa ajili ya vipimo vya afya endapo makubaliano yatafikiwa.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa yupo La Manga, Hispania, akiwa na Newcastle kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya. Guimaraes ambaye ni nahodha wa Newcastle amekuwa akionyesha heshima kwa klabu hiyo na hakuwahi kushinikiza kuondoka.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil ameeleza kuwa angependa kujiunga na Arsenal iwapo klabu hizo zitakubaliana kuhusu ada na masharti ya uhamisho.
Newcastle United bado ina matumaini ya kumbakiza Guimaraes, ambaye ana miaka miwili iliyosalia kwenye mkataba wake pamoja na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Arsenal inaona Guimaraes kama mchezaji muhimu anayeweza kuongeza nguvu katika eneo la kiungo, huku mazungumzo yakiendelea kati ya klabu hizo mbili katika kipindi hiki cha usajili.