Brazil Yaifunga Haiti 3-0 na Kukaribia Kufuzu Hatua ya Mtoano Kombe la Dunia 2026

Brazil imefufua matumaini yake ya kufanya vizuri katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Haiti mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi C uliochezwa Philadelphia.

Nyota wa mchezo alikuwa Matheus Cunha, aliyefunga mabao mawili muhimu yaliyoiwezesha Brazil kupata ushindi wake wa kwanza kwenye mashindano hayo baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Morocco katika mchezo wa ufunguzi.

Cunha alianza kuiandikia Brazil bao la kwanza dakika ya 23 kabla ya kuongeza la pili kwa shuti kali kufuatia pasi kutoka kwa Vinicius Junior. Vinicius naye aliandika jina lake kwenye orodha ya wafungaji kwa kufunga bao la tatu kabla ya mapumziko.

Kocha Carlo Ancelotti alifanya mabadiliko kadhaa baada ya mchezo wa kwanza uliokosolewa na wengi, na Brazil ilionyesha tofauti kubwa dhidi ya Haiti ambao sasa wamekuwa taifa la kwanza kuaga rasmi Kombe la Dunia 2026.

Haiti walipata nafasi chache za kushtua lango la Brazil, huku kipa Alisson Becker akifanya kazi nzuri kuzuia juhudi zao na kuisaidia Brazil kupata clean sheet yake ya kwanza katika michezo saba iliyopita.

Matokeo hayo yanaifanya Brazil kufikisha pointi nne sawa na Morocco, lakini ikiongoza Kundi C kutokana na tofauti ya mabao. Brazil sasa itakutana na Scotland katika mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi Juni 24, huku Haiti wakimalizia kampeni yao dhidi ya Morocco.