Rais wa Kenya, William Ruto, amesema ameialika klabu ya Arsenal kutembelea Kenya baada ya kushuhudia namna mashabiki wa timu hiyo walivyosherehekea ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa shamrashamra kubwa nchini humo.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa G7 uliofanyika nchini Ufaransa, Ruto alisema alishangazwa na ukubwa wa sherehe zilizofanyika jijini Nairobi na maeneo mengine nchini Kenya kufuatia Arsenal kutwaa taji la ligi baada ya kusubiri kwa muda mrefu.

“Arsenal hatimaye ilipata ubingwa, na kuwa sherehe kubwa. Nilishangaa sana kilichotokea jijini Nairobi,” alisema Ruto.
Rais huyo alibainisha kuwa tayari ametuma mwaliko kwa klabu hiyo ya Kaskazini mwa London ili ifanye ziara nchini Kenya mwaka ujao, akiamini kuwa hatua hiyo itakuwa zawadi kwa mamilioni ya mashabiki wa Arsenal waliopo nchini humo.
“Ilikuwa sherehe kubwa. Najaribu kufuatilia kama Arsenal wanaweza kuja nchini mwaka ujao. Nimetuma mwaliko kwa sababu nafikiri itakuwa wakati mzuri kwa Arsenal kuja Kenya. Wana mashabiki wa kipekee,” aliongeza.