Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, ameandika historia nyingine usiku wa kuamkia leo baada ya kufunga mabao matatu (hat-trick) na kuiongoza Argentina kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Algeria katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia.
Mashabiki wengi walikuwa wakisubiri kuona mchango wa Messi mwenye umri wa miaka 39 katika mashindano hayo ambayo yanatajwa kuwa ya mwisho kwa nyota wengi wa soka duniani. Kabla ya mchezo huo, Kylian Mbappe alikuwa ameongeza mabao yake katika historia ya Kombe la Dunia kwa kufunga mara mbili, lakini Messi alihakikisha anarejesha mjadala kwake kwa kiwango cha juu kabisa.
Dakika za mwanzo zilishuhudia timu zote zikifunga mabao yaliyokataliwa kwa kuotea. Messi alitikisa nyavu dakika ya tano kabla ya bao hilo kufutwa, huku Algeria pia wakifunga kupitia Fares Chaibi lakini nao wakakataliwa.
Messi hakusubiri sana kurekebisha hali hiyo. Dakika ya 17 alipokea pasi kutoka kwa Rodrigo De Paul na kufunga bao la kwanza kwa shuti la ustadi lililomshinda kipa Luca Zidane.
Bao hilo lilimfanya Messi kuwa mchezaji wa kwanza kushiriki Kombe la Dunia mara sita na pia kufunga katika mashindano matano tofauti ya Kombe la Dunia.
Kipindi cha pili kilimshuhudia Messi akiendelea kutawala mchezo. Dakika ya 60 alifunga bao lake la pili baada ya kipa Zidane kushindwa kudhibiti mpira uliopigwa na Alexis Mac Allister.
Dakika ya 76, Messi alikamilisha hat-trick yake kwa shuti la chini kutoka nje kidogo ya eneo la hatari na kuisogeza Argentina mbele kwa mabao 3-0.
Baada ya kufunga bao hilo, Messi alisawazisha rekodi ya mabao mengi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia iliyokuwa ikishikiliwa na Miroslav Klose.
Mwishoni mwa mchezo, Messi alitolewa nje huku mashabiki wa pande zote wakisimama kumpigia makofi na kuimba jina lake, katika usiku ambao utaendelea kukumbukwa na mashabiki wa soka duniani.
Kwa upande wa Algeria, ilikuwa ni mwanzo mbaya wa kampeni yao ya Kombe la Dunia baada ya kurejea kwenye mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014.