Kundi la wawekezaji kutoka Qatar lililowahi kujaribu kuinunua Manchester United halijawasiliana tena na uongozi wa klabu hiyo, licha ya taarifa zinazoendelea kusambaa kuwa baadhi ya familia ya Glazer wanataka kuuza hisa zao.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, hata kama kundi hilo lingefuatwa kwa ajili ya mazungumzo mapya, uwezekano wa kurejea mezani kuwasilisha ofa nyingine kwa sasa ni mdogo sana.
Uvumi kuhusu familia ya Glazer kutaka kuondoka Old Trafford umeendelea kwa muda mrefu, huku ripoti ya Bloomberg ikidai baadhi ya wanafamilia wanataka kuuza sehemu yao ya umiliki baada ya zaidi ya miaka 20 kuiongoza klabu hiyo.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya klabu vimeripotiwa kupinga taarifa hizo, huku Manchester United wakikataa kutoa maoni rasmi kuhusu suala hilo.
Mwaka 2023, kundi la Qatar lililoongozwa na Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani liliwasilisha ofa ya takribani pauni bilioni 5 kwa ajili ya kununua umiliki wote wa Manchester United.
Lakini badala yake, familia ya Glazer waliamua kuuza asilimia 25 ya hisa za klabu kwa bilionea wa Uingereza Jim Ratcliffe kupitia kampuni yake ya INEOS kwa kiasi cha pauni bilioni 1.3.
Inaelezwa kuwa kundi hilo la Qatar bado lina maumivu kutokana na mchakato wa awali wa mauzo na kwa sasa halina nia ya kurejea kwenye mazungumzo ya kuinunua klabu hiyo.
Baada ya uwekezaji wa Ratcliffe, alipewa mamlaka ya kusimamia shughuli za kiutendaji ndani ya klabu, ambapo ameanzisha mabadiliko mbalimbali ikiwemo kupunguza matumizi na nafasi za kazi.
Taarifa za kifedha za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Manchester United imepata faida ya uendeshaji ya pauni milioni 37.7 katika kipindi cha miezi tisa hadi Machi mwaka huu.
Klabu hiyo pia inaendelea kujadili iwapo ijenge uwanja mpya wenye uwezo wa mashabiki 100,000 au ifanye maboresho makubwa katika dimba la Old Trafford.