Klabu ya Paris Saint-Germain imefanikiwa kutwaa taji la pili mfululizo la UEFA Champions League baada ya kuifunga Arsenal kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 kwenye fainali iliyochezwa Budapest.
Ilikuwa ni usiku wa majonzi kwa Arsenal huku beki Gabriel akiwa mhusika mkuu wa huzuni hiyo baada ya kukosa penalti ya mwisho iliyowapa PSG ushindi mkubwa wa Ulaya.
Arsenal walianza mchezo kwa kasi na kufunga bao la mapema dakika ya sita kupitia Kai Havertz aliyemalizia vizuri pasi iliyotokana na makosa ya safu ya ulinzi ya PSG. Bao hilo liliwapa matumaini makubwa mashabiki wa Gunners waliokuwa wakisaka historia ya kutwaa mataji mawili makubwa msimu huu.

Katika dakika nyingi za mchezo huo, Arsenal walionekana kucheza kwa nidhamu kubwa ya kujilinda huku Gabriel akiwa nguzo muhimu kabisa ya safu ya ulinzi. Beki huyo wa Brazil alifanya kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi ya PSG kwa kuokoa mipira mingi ya hatari na kuiongoza timu yake kwa utulivu mkubwa.
Hata hivyo, kipindi cha pili PSG waliinuka na kuanza kushambulia kwa nguvu zaidi hadi walipopata penalti baada ya Cristian Mosquera kumuangusha Kvicha Kvaratskhelia ndani ya eneo la hatari. Ousmane Dembele hakufanya makosa na kusawazisha mchezo huo.
Baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 1-1, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Kipa David Raya aliweka matumaini kwa Arsenal baada ya kuokoa penalti ya Nuno Mendes lakini matumaini hayo yalizimika Gabriel alipokosa mkwaju muhimu uliopaa juu ya lango.
Mara baada ya penalti hiyo kukosa, wachezaji wa PSG waliinuka kwa shangwe kubwa huku Arsenal wakibaki na majonzi makubwa ya kupoteza fainali nyingine ya Champions League, miaka 20 tangu walipopoteza dhidi ya Barcelona mwaka 2006.
Kocha wa PSG Luis Enrique ameendelea kuandika historia akiwaongoza mabingwa hao wa Ufaransa kutwaa ubingwa mwingine mkubwa wa Ulaya, huku kocha wa Arsenal Mikel Arteta akibaki kusubiri ndoto yake ya kwanza ya Champions League.
