Crystal Palace Yatwaa UEFA Conference League Kwa Mara ya Kwanza

Klabu ya Crystal Palace F.C. imeandika historia mpya baada ya kutwaa taji la UEFA Europa Conference League kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayo Vallecano katika mchezo wa fainali uliochezwa Jumatano Mei 27, 2026 kwenye Uwanja wa Red Bull Arena Leipzig nchini Germany.

Bao pekee la ushindi lilifungwa na mshambuliaji Jean-Philippe Mateta katika dakika ya 51, bao lililoihakikishia Crystal Palace taji lake la kwanza kabisa la mashindano ya Ulaya.

Ushindi huo pia umekuwa wa kihistoria kwa meneja wa timu hiyo Oliver Glasner ambaye ameiongoza Crystal Palace kutwaa mataji matatu ndani ya kipindi kisichozidi miezi 12 kabla ya kuondoka rasmi klabuni hapo baada ya mchezo huo.

Mbali na kutwaa Conference League, Glasner aliiongoza Crystal Palace kushinda Kombe la FA msimu uliopita pamoja na Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu.

Kutokana na ubingwa huo, Crystal Palace sasa imejihakikishia nafasi ya kushiriki UEFA Europa League msimu ujao.

Aidha, Crystal Palace imekuwa timu ya pili kutoka England kutwaa taji la Ulaya msimu huu baada ya Aston Villa F.C. kufanya hivyo katika michuano ya Europa League.

England sasa ina nafasi ya kuandika historia ya kuwa na klabu tatu zilizotwaa mataji yote matatu ya Ulaya katika msimu mmoja iwapo Arsenal F.C. itaifunga Paris Saint-Germain F.C. kwenye fainali ya UEFA Champions League itakayochezwa Jumamosi.