Manchester United Yamthibitisha Michael Carrick Kuwa Kocha Mkuu

Manchester United wamefikia makubaliano ya kumteua Michael Carrick kuwa kocha mkuu wa kudumu wa klabu hiyo baada ya kufanya vizuri tangu apewe jukumu la muda mwezi Januari.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, taratibu rasmi za kubadilishana mikataba zinaendelea kwa sasa huku tangazo rasmi likitarajiwa kutolewa ndani ya saa 48 zijazo. Hata hivyo, bado haijafahamika kama mchakato huo utakamilika kabla ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Nottingham Forest, lakini viongozi wa klabu wana matumaini ya kumaliza kila kitu kabla ya mchezo wa mwisho wa nyumbani msimu huu.

Carrick anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 ameonyesha mafanikio makubwa tangu aliporithi mikoba ya Ruben Amorim ambaye alifutwa kazi mwezi Januari.

Tangu achukue mikoba hiyo, Carrick ameiongoza Manchester United kushinda michezo 10 kati ya 15 ya Premier League na kuisaidia timu hiyo kufuzu kucheza UEFA Champions League msimu ujao.

Ripoti zinaeleza kuwa viongozi wakuu wa klabu hiyo akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu Omar Berrada pamoja na Mkurugenzi wa Soka Jason Wilcox waliwasilisha mapendekezo kwa wamiliki wa klabu, INEOS, ili Carrick apewe nafasi hiyo moja kwa moja, jambo ambalo limekubaliwa rasmi na uongozi wa juu wa klabu hiyo.

Mashabiki wengi wa Manchester United wamekuwa wakionesha imani kubwa kwa Carrick kutokana na namna alivyoleta mabadiliko makubwa ndani ya kipindi kifupi tangu apewe timu hiyo kwa muda.