Serikali Yatoa Bonasi kwa Twiga Stars Baada ya Kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika

Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, imekabidhiwa bonasi ya shilingi milioni 50 Disemba 3, 2025 kama pongezi ya mafanikio yao ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika ya Wanawake (WAFCON) 2026.

Bonasi hiyo imetolewa na Msemaji wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, akisema kuwa heshima hiyo ni sehemu ya kutambua jitihada, kujituma na mafanikio ya kikosi cha Twiga Stars.

“Twiga Stars mmeonyesha ubora na kujituma kwa kiwango cha juu, na Serikali inathamini mchango wenu katika kuboresha hadhi ya Tanzania kwenye michezo ya kikubwa barani Afrika. Bonasi hii ni pongezi kwa mafanikio yenu,” alisema Msigwa wakati wa kukabidhi bonasi hiyo.

Hii ni hatua nyingine muhimu inayojumuisha jitihada za Serikali katika kukuza michezo ya wanawake nchini, huku Twiga Stars wakisonga mbele kwa matarajio ya kuwakilisha Tanzania kwa heshima kwenye mashindano ya WAFCON 2026.