Home Uncategorized MBWANA SAMATTA AHESHIMIWE, KAZI YAKE NI KUBWA

MBWANA SAMATTA AHESHIMIWE, KAZI YAKE NI KUBWA

“UKIKUBALI ujinga upewe nafasi werevu utapotea mithili ya moshi angani.” Kauli hii alikuwa anapenda kuitumia Mwalimu Dkt. Thadei Mwereke pale Chuo Kikuu cha Kampala ambapo niliwahi kusoma pale. Hii inamaanisha kwamba kamwe tusiruhusu ujinga kupenya kwenye dunia ya werevu.

Mbwana Samatta moja ya tunu na fahari ya taifa letu bahati mbaya sana amejikuta kwenye dunia ambayo ujinga unapewa nafasi kubwa kuliko weledi. Kumeibuka mijadala ya kipuuzi kuhusu nahodha wetu Mbwana Samatta kuwa hatoshi na hafai kuwa sehemu ya kikosi cha Stars nikiri wazi mimi ni miongoni mwa wadau ambao nimesikitishwa na kauli hizi kumhusu nahodha wetu Mbwana Samatta.

Nani asiyefahamu kuwa Samatta ni kielelezo na role model wa vijana wengi wapambania ndoto kwenye mchezo wa soka nchini? Kila mzazi alitamani mwanae awe Samatta ajaye kutokana na alama aliyoiweka Captain Diego kwenye kila nyasi alizokanyaga kuanzia pale DR Congo, Ubelgiji, England, Uturuki na sasa Ugiriki akikipiga na miamba Paok FC.

Jambo la kushangaza leo hii kinaibuka kikundi cha wahuni ambao wana uwezo wa kuchapisha maoni instagram na facebook wanaanza kumdhihaki Samatta ambaye ni fear factor kwa kila mpinzani anayekuja kucheza na Stars jina la kwanza kulifikiria kichwani mwake ni Mbwana. Ubora ambao ameuonyesha Samatta umekuwa fimbo kwa wapinzani na kama nyota wa Stars wangetumia vizuri mwanya huu ni wazi mabao mengi yangepatikana kupitia mgongo wa Poppa.

Samatta amekuwa mchezaji wa kuchungwa zaidi kwenye kikosi cha Stars kuliko mchezaji yoyote, Stars tumefunga bao moja kwenye michuano ya Afcon asisti pekee ya Captain Diego cha kushangaza bado hatuoni umuhimu wake, Samatta akiwa Stars anatimiza majukumu lukuki ndani ya uwanja, atacheza kama kiungo wa pembeni, kiungo wa kati na mshambuliaji kwa wakati mmoja lakini wengi hatulioni kwa kujivika upofu tusokuwa nao.

Kila ndoto ya kijana mcheza soka kwa kizazi chetu matarajio, shauku na matamanio yake ni kufika alipofika Mbwana Samatta mchezaji pekee Mtanzania mwenye tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani. Nina swali moja kwenu wajuaji wa soka mnaosema Captain hajitumi, hao waliojituma kabla yake walitufikisha wapi kama nchi, tulifuzu Afcon ngapi?,

 Tulishinda mechi ngapi Afcon? Tukiwa na huyu ambaye hajitumi hadi sasa tumeshuhudia Afcon mbili akiwa na kitambaa cha unahodha kwenye mkono wake na asilimia zaidi ya 70 ya mabao kwenye mechi za kufuzu yalitokana na jitihada zake jambo ambalo liliwarahisishia akina Msuva kutupia kambani bila bugdha yoyote.

Tumpe heshima yake Captain Samatta, tupunguze ujuaji kwenye mambo ambayo hatuyajui pia tusijikite kwenye kichaka cha maoni kwa kusapoti ujinga ambao tunaweza kuuepuka. Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo kila mtu ni refa, kocha, mtaalamu wa tiba za wachezaji, mwanasheria, mchambuzi na kadhalika jambo ambalo linazidi kupalilia mambo ya kipuuzi kupewa muda zaidi kuliko weledi. Go Stars go Captain Diego.

Ameandika Hussen Msoleka.

Karibuni Temeke.

Previous articleAMETAJA SIKU YA NYOTA SIMBA KUTUA
Next articleNYOTA HUYU SIMBA KUIBUKIA RAJA CASABLANCA