UHISPANIA, URENO NA MOROCCO WATHIBITISHWA KUWA WENYEJI KOMBE LA DUNIA 2030

Shirikisho la soka Duniani (FIFA) limethibitisha kuipatia Saudi Arabia haki za kuwa nchi mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA la 2034 huku Uhispania, Ureno na Morocco wakithibitishwa kuwa wenyeji wenza wa kombe la Dunia la mwaka 2030

Uamuzi huo umetolewa wakati wa mkutano wa FIFA leo huku mashindano hayo yakitarajiwa kufanyika wakati wa miezi miwili ya baridi ili kuepuka joto kali la kiangazi kama iliyofanyika wakati wa Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.

Aidha michuano ya Kombe la Dunia la 2030 itazishuhudia Mataifa ya Uruguay, Argentina na Paraguay zikiandaa mechi moja kila moja.

Wakati uamuzi huo ukifikiwa Rais wa FIFA, Gianni Infantino alihoji: “Ni njia gani bora ya kusherehekea miaka 100 ya Kombe la Dunia kuliko hii ya kuwa na Kombe la Dunia katika nchi sita, katika mabara matatu na timu 48?”

Mechi tatu za ufunguzi wa michuano hiyo ya 2030 zitapigwa nchini Uruguay, Argentina na Paraguay huku FIFA ikipanga kusherehekea miaka 100 tangu Kombe la Dunia la kwanza. Mechi zingine zilizosalia zitaandaliwa kati ya Morocco, Ureno na Uhispania.