Home Uncategorized KILA LA KHERI TAIFA STARS

KILA LA KHERI TAIFA STARS

USHINDANI ni mkubwa na kila timu inafanya kweli kupata ushindi ndani ya uwanja hivyo muhimu ni kujituma na kupata matokeo chanya.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo ina kibarua kingine kigumu kusaka ushindi dhidi ya DR Congo hautakuwa mchezo mwepesi hata kidogo.

Kila timu inatafuta pointi tatu hivyo ni muhimu kwa wachezaji kujituma bila kuogopa na mwisho kuwapa furaha Watanzania.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jukumu lenu ni moja kusaka ushindi uwanjani hatua ya makundi ushindi bado haujapatikana hivyo ni muhimu kupata ushindi.

Kuanza kwa kupoteza mchezo wa kwanza wa Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), dhidi ya Morocco kisha sare dhidi ya Zambia haikuwa mwendelezo mzuri lakini ni matokeo.

Inatokea na inaumiza kulingana na vile ambavyo wachezaji mlijituma zile presha za mashabiki kwamba muda wenu umegota mwisho, zibebeni kwa mikono miwili na kuwapa matokeo yale wanayoyapenda.

Matokeo wanayoyapenda mashabiki yatawaongezea furaha maradufu, huku mkizidi kudumu kwenye ule ubora wenu na maajabu yenu ambayo yapo kwenye miguu yenu.

Kila mmoja ana nafasi ya kufanya vizuri na kuamini kwamba kama kuna siku ya kukosa basi na ile ya kupata ipo pia jambo la msingi ni kuendelea kupambana bila kuchoka.

Wakati uliopo ni sasa kupambana dhidi ya DR Congo uimara na kushirikiana pamoja na kupunguza makosa viwe nguzo kwenu. Kila la Kheri Tanzania.

Previous articleMITAMBO YA MABAO AZAM FC HII HAPA
Next articleAMETHIBITISHA BALAA LA MBEBA MIKOBA YA BALEKE SIMBA