LAKINI SIMBA MNA UHAKIKA TATIZO NI ROBERTINHO?

MWANAMUZIKI mkazi wa mkoani Morogoro, Selemani Msindi ‘Afande Sele’ aliwahi kuimba ‘kama hip-hop itakufa ni nani anapaswa kuchunwa ngozi? Je, ni Producer, mapromota au wasanii?’

Tungo hii ilikuwa na ujumbe kuwa ni lazima atafutwe wa kuwajibika kutokana na kudorora na ikitokea mziki huo wa ‘kufokafoka’ ukafa, hasa baada ya mziki wa aina ya Bongo Fleva kuja juu.

Kwanini nimeanza na tungo ya Afande Sele? Ni hivi   moto unawaka Simba! katika hali isiyotarajiwa jana Jumanne mchana uongozi wa Simba kupitia mitandao yao ya kijamii uliushitua umma wa Watanzania baada ya kutoa taarifa ya kufikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu Mbrazili, Robert Olivieira ‘Robertinho’.

Mshtuko huo ulitokana na ukweli kuwa kocha huyo amehudumu kwa kipindi cha miezi 10 tu, ndani ya Simba mara baada ya kutangazwa rasmi kuwa kocha mkuu mwezi Januari mwaka huu.

Ukiachana na hilo maswali yanazidi kuwa mengi pale unapokumbuka kuwa Robertinho ameachana na Simba huku akiwa ametoka kupokea tuzo ya kuwa kocha bora wa mwezi Oktoba na akiwa amepoteza mchezo mmoja tu, wa Ligi Kuu Bara tangu achukue mikoba ya kuiongoza Simba.

Ikumbukwe kuwa Robertinho alichukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa Simba, Zoran Maki ambaye aliachana na Simba baada ya kuiongoza kwa siku 60 tu, kabla ya kutimkia nchini Misri na timu kuachiwa Juma Mgunda.

Taarifa za ndani ya Simba zinaeleza kuwa, kulikuwa na hali ya sintofahamu kati ya baadhi ya watendaji wa timu hiyo kwa maana ya uongozi, benchi la ufundi la timu hiyo na baadhi ya wachezaji.

Kipigo cha mabao 5-1 siku ya Jumapili ndiyo inatajwa kuwa sababu kubwa ambayo imechangia kufukuzwa kwa kocha huyo, huku presha ikizidi kuwa kubwa kutokana na  timu hiyo msimu huu kuonekana ikicheza chini ya kiwango licha ya usajili mkubwa walioufanya.

Maamuzi magumu ni suala ambalo lilitarajiwa kutokea kutoka kwenye uongozi wa Simba, lakini swali kubwa ni je, hatua hiyo pekee ndiyo itamaliza hali ya mambo ndani ya kikosi chao?

Bila shaka ukifikia hatua hiyo utakubaliana nami kuwa Robertinho sio tatizo pekee la Simba, kumeonekana kuwa na changamoto kubwa ya ufiti wa wachezaji wa timu hiyo, huku sehemu kubwa ya usajili uliofanyika pia ukishindwa kufikia matarajio, hapo achana na tatizo la majeraha.

Lakini vipi kuhusu ishu ya mahusiano ya baadhi ya viongozi na wachezaji kama inavyoelezwa?

Kama utaangalia makosa ni mengi na huenda yamesababishwa na sehemu fulani kama siyo yote ya Uongozi wa Simba, kwani maamuzi ya kusajili au kuachana na mchezaji si jambo la mtu mmoja bali Uongozi wa klabu kwa ujumla wake.

Kuendana na tungo ya, Afande Sele nadhani Simba wao wameamua kumchuna ngozi Robertinho, lakini nadhani wana safari ndefu ya kufanya maamuzi kuhakikisha wanarejesha makali yao.

Hii ni kwa sababu katika uhalisia wa mambo kuna namna kila mmoja ndani ya taasisi yao amehusika na matokeo ya klabu yao kukosa muelekeo.

Wakati Robertinho ametolewa kafara ili kupata utulivu, nadhani Simba sasa wanatakiwa kufanya kazi kubwa kuiokoa meli yao ili isizidi kwenda mrama na kama wataleta masikhara basi makubwa yatawakuta.