HIVI NDIVYO SIMBA WALIVYOLOWA KWA MKAPA MBELE YA MASHABIKI WAO

MWENDO wa 5G mkono ulikuwa jana Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi ambapo baada ya dakika 90 ilikuwa Simba 1-5 Yanga.

Ni Yanga walianza kupata bao la kuongoza mapema kabisa dakika ya tatu kupitia kwa Kennedy Musonda ambaye alitumia pasi ya Yao Attohoula aliyemwaga
majalo ndani ya 18.

Kipindi cha pili Yanga walianza kwa kasi wakianza kupachika bao la pili dakika ya 64 kupitia kwa Maxi Nzengeli aliyefunga bao lingine dakika ya 77.

Aziz KI alipachika bao moja dakika ya 73 huku msumari wa tano kwa Yanga ukijazwa kimiani na Pacome Zouzoua dakika ya 87 kwa mkwaju wa penalti baada ya beki Che Malone kumchezea faulo mshambuliaji Mzize Clement
ambaye alianzia benchi.

Sio mara ya kwanza kwa Yanga kushinda mabao matano, waliwatungua KMC, JKT kwenye mechi zilizochezwa Uwanja wa Azam Complex jana ilikuwa ni zamu ya watani
zao wa jadi Simba.

‘Wameloooowa’ zilikuwa ni tambo za mashabiki wa Yanga waliojitokeza Uwanja wa Mkapa wakishangilia ushindi huo kwa kukomba pointi tatu mbele ya Simba.

Miguel Gamondi kavunja rekodi ya kocha wa Simba Roberto Oliveira ambaye alikuwa hajapoteza mchezo wowote ndani ya ligi.

Aishi Manula kaanza siku yake ikiwa ni mkosi kwake kwa kuwa alitunguliwa mabao matano kwenye mchezo huo ambao ulikuwa ni wa kwanza msimu wa 2023/24.

Ni Kibu Dennis alipachika bao pekee kwa Simba dakika ya 8 akitumia pasi ya Saido Ntibanzokiza ambaye alipiga kona ndefu kipindi cha kwanza mabeki wa Yanga walipokuwa kwenye harakati za kuokoa hatari.

Kuumia kwa Kibu dakika ya 59 na nafasi yake
kuchukuliwa na Luis Miquissone kulibadili upepo kwa Simba ambao walionekana kushindwa kutengeneza nafasi kuelekea kwenye lango la Yanga.

Hiki ni kichapo kikubwa kwa Simba kukipokea msimu wa 2023/24 ukiwa ni mchezo wa kwanza kwao kupoteza ndani ya ligi baada ya kucheza mechi sita bila kufungwa.

Licha ya mvua kunyesha siku ya jana kwenye maeneo tofauti ya Dar, bado mashabiki walijitokeza kwa wingi uwanjani kushuhudia mchezo huo mkubwa Afrika.

Kocha Mkuu, Roberto Oliveira alianza na kikosi cha kwanza namna hii:-Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Che Malone, Fabrice Ngoma, Kibu Dennis, Sadio Kanoute, Baleke, Saido
Ntibanzokiza, Clatous Chama.

Miguel Gamondi Kocha Mkuu wa Yanga yeye alianza namna hii:- Djigui Diarra, Yao Attouhula, Joyce Lomalisa, Bacca,Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudhathir Yahya,
Kennedy Musonda, Aziz Ki, Pacome Zouzoua.