Home Sports SIMBA YAWAPIGIA HESABU WAZAMBIA KIMATAIFA

SIMBA YAWAPIGIA HESABU WAZAMBIA KIMATAIFA

KOCHA Mkuu wa Simba Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema wameutumia mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union uliopigwa Alhamisi iliyopita kama sehemu ya kujiandaa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Mbali na mchezo huo pia Simba ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Pan African na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 yote ikiwa ni maandalizi kuelekea mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa.

Robertinho ameweka wazi kuwa katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union aliwatumia wachezaji wenye uzoefu, ili kuzidi kutengeneza maelewano baina yao kuelekea mechi dhidi ya Power Dynamos itakayopigwa Jumapili.

Simba Jumapili watashuka uwanjani na Dynamos katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya hatua ya makundi ya mashindano hayo, ikumbukwe mchezo wa kwanza ambao Simba walicheza ugenini nchini Zambia, Simba walipata matokeo ya sare mabao 2-2.

 Robertinho amesema: “Tumeutumia mchezo dhidi ya Coastal Union kujiandaa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos. Tulijua Coastal watatupa mechi ngumu ambayo itazidi kutuimarisha.

 “Ukiangalia kikosi cha mchezo ule kwa kiasi kikubwa tumewatumia wachezaji wenye uzoefu ambao tunategemea kuwatumia dhidi ya Power Dynamos.”

Previous articleKOCHA AL MERRIKH: YANGA INAOGOPESHA
Next articleAZAM FC WANA JAMBO LAO