TUSIJUMUISHE USHABIKI KWENYE MASUALA YA KUUMIZWA KWA INONGA

WAKATI mwingine si vibaya kusema mashabiki wa mpira na hasa Tanzania wamekuwa na mambo mengi sana yanayopaswa kulaaniwa.

Binafsi nayaona ni masuala ambayo yanaonyesha ushabiki kupindukia wakati mwingine unakuwa ni tatizo kubwa sana.

Ushabiki wa aina hiyo umewafanya mashabiki wengi washindwe kujitambua na ndio maana umeona baadhi ya mashabiki au wahamasishaji wanaotangaza zaidi chuki wamekuwa maarufu sana.

Wamekuwa ni watu ambao wanaonekana ni watu wa maana sana kwa kuwa mashabiki kadhaa ndicho wanachokiamini au kukitaka.

Mhamasishaji madala ya kuzungumzia mazuri ya klabu yake, anazungumzia mabaya ya klabu nyingine na muda mwingi anawajaza chuki mashabiki wake dhidi ya mashabiki wa klabu nyingine ambalo ni jambo hatari sana.

Hili limekwenda linashuka taratibu na mimi nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba jambo hili linapaswa kuanza kukemewa sasa na si baadaye.

Tunavyoendelea kuliacha, lianzidi kuchukua eneo kubwa na hii inakwenda kuwa hatari hapo baadaye katika mpira wetu na taifa kwa ujumla.

Angalia sasa mambo yanavyokuwa, kaumizwa vibaya beki wa Simba, Inonga Baka, ilikuwa ni ajali kazini dhidi ya Haji Ugando wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ajabu zaidi, mashabiki mjadala wao ni kuwa “hakuumia”, “kajifanyisha”, “anapenda kuonekana”, na unashangazwa kuona shabiki au mashabiki wanaozungumza ni watu wenye familia zao.

Nasema wenye familia zao kwa kuwa kila unapopata majukumu na kuwa kiongozi wa familia, Imani na uelewa wa maumivu ya wengine unapanda kwa kiasi kikubwa zaidi.

Hawa hawaelewi, wanazungumza kama Watoto wadogo wakati hata aliyefanya faulo tu na wachezaji wengi wa Coastal Union walichanganyikiwa.

Ajabu, mtu mwingine anaona ni tukio la kuigiza licha ya kuwepo kwa Ushahidi wa kutosha wa video. Mijadala baada ya tukio hilo kwa asilimia kubwa imejaa utoto badala ya uhalisia.

Mchezaji hata kama si wa timu yako, anapoumia unaangalia zaidi ubinadamu kwa kuwa hapo inakuwa imevuka level ya ushabiki na niwakumbushe kuwa burudani haiwezi kuwa bora zaidi ya ubinadamu.

Msimu uliopita aliumizwa Moses Phiri, katika mijadala ilikuwa ni hivyohivyo, “anajifanyisha”, “asiumizwe yeye nani” na maneno mengi ya kejeli.

Anayeumizwa vipi unamkejeli, unakumbuka naye ni binadamu? Unakumbuka huyu ni mtu mwenye watu wanaimtegemea wakiwemo wazazi? Sasa vipi tunakosa ubinadamu hivyo?

Wakati Fulani niliwahi kukemea faulo ya kipuuzi aliyoifanya Serge Wawa akiwa Simba, alimfanyia Ditram Nchimbi. Cha kushangaza, wachangiaji badala ya mjadala wakawa wanakumbusha faulo kadhaa za wachezaji wa Yanga.

Haukuwa mjadala faulo zile, lakini Wawa kupanda juu ya mguu wa Nchimbi halikuwa jambo la kiungwana. Na hakukuwa na haja ya kulipishiana kwa kuonyesheana.

Lazima tuungane, tubadilike na kwa mashabiki basi lazima mjue kiwango na urefu wa Kamba ya ushabiki wa mpira inapoishia na wapi ubinadamu au utu unaingia.

Dhihaka katika maumivu ya binadamu mwenzako ni utoto wa kiwango cha juu sana.

Kama utakuwa shabiki wa mpira na unashindwa kulitambua hilo, basi kunakuwa na walakini mkubwamkubwa sana.

Walioanzisha Yanga na Simba walikuwa bora kuliko sisi na utambuzi wao wa ushabiki wa mpira uliwapa faida nyingi kubwa ikiwemo kuwaunganisha na kadhalika.

Ndio maana ulikuwa ukisikia, mfano Simba na Yanga ambao ni watani wa jadi (si mahasimu), wamekuwa wakishirikiana sana katika masuala mengi ya kijamii.

Wakati msiba unamhusisha mtu wa Simba, basi Yanga ndio wanasimamia mazishi na upande wa Yanga hali kadhalika.

Haya yote yamepotea kwa kuwa ushabiki wa kitoto umechukua nafasi kubwa wakati huu na kupoteza kabisa ubinadamu au utu ndani yake na hili tunapaswa tulikemee kwa nguvu sana na kurekebisha mambo ili kuufanya mpira uzidi kutuunganisha na faida ya utu na ubinadamu izidi kuimarika na kupanda ndani yetu.