MWAMBA wa Lusak, Clatous Chama gari limeweka kutokana na kasi yake ya kufunga na kutengeneza mabao kuanza kurejea kwa namna yake.
Ikumbukwe kwamba msimu wa 2022/23 Chama alikuwa ni namba moja kwa viungo waliotoa pasi nyingi ndani ya ligi ambazo ni 14.
Msimu wa 2023/24 pasi yake ya kwanza aliitoa kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union uliochezwa Uwanja wa Uhuru na baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 3-0 Coastal Union.
Wakati akifungua akaunti ya pasi za mabao Chama alitoka kuonyesha makeke yake kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Levy Mwanawasa, Chama alipachika mabao mawili akiwa ni nyota wa mchezo huo wa kusaka hatua ya makundi.
Deni lake kwenye ligi ni pasi 13 huku akiwa na kazi nyingine kushirikiana na wachezaji wote wa timu ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kusaka ushindi mchezo wa marudiano dhidi ya Power Dynamos kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.