Home Uncategorized UKUBWA WA SIMBA UMESHAFAHAMIKA

UKUBWA WA SIMBA UMESHAFAHAMIKA

INAKUJA African Super League ambayo itashirikisha timu kubwa nane tu za Afrika kutoka katika kila ukanda wa bara hilo.

Upande wa Afrika Mashariki, kigogo wa ukanda wetu ni Simba ambao ndio wanawakilisha ukanda wote.

Simba ndio timu kubwa na maarufu zaidi katika ukanda wa Cecafa na hasa unapozungumzia masuala yanayohusu Shirikisho la Soka Afrika na michuano yake.

Simba imekuwa na mabadiliko makubwa katika misimu saba iliyopita na ndio timu ya ukanda wa Mashariki iliyoshiriki na kufanya vizuri zaidi katika michuano iliyo chini ya Caf.

Kuna mjadala umekuwa ukiendelea hapa nchini na huu mara nyingi unatokana na ule ushabiki wa watani Yanga na Simba na kila mmoja akitaka kuonyesha ni mkubwa sana kuliko mwenzake.

Huenda mjadala huanzishwa kwa maana ya kila mmoja kutaka kuwa juu lakini katika suala la namba ambalo huamua ukubwa wa mpira limekuwa halina ubishi.

Mijadala ya kuundwa kwa makusudi kupotosha uhalisia imekuwa ni mingi sana lakini haina faida kwa kuwa mara nyingi imekuwa ikiangukia pua kutokana na uhalisia.

Huu ni uhalisia mwingine tena, Simba inashiriki African Super League na inakusanya hadi Sh bilioni 5 kwa ajili ya maandalizi tu.

Fedha ambazo ni vigumu kuona hata mabingwa wa michuano mikubwa ya Caf wanachukua. Simba wako na timu nyingine saba ambazo ni Al Ahly ya Misri, Wydad ya Morocco, Esperance ya Tunisia, Enyimba ya Nigeria, Mamelodi ya Afrika Kusini, Atletico ya Angola na TP Mazembe ya DRC.

Tayari Simba imepangwa na Al Ahly kuanza michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika. Simba inaingia kwenye rekodi ya kuwa moja ya timu zilizofanikiwa kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza ikifanyika barani Afrika na hii itabaki kwa muda mrefu sana katika historia ya mpira.

Achana na hivyo, umeona hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambako Simba na Yanga ndio wawakilishi wa Tanzania, Yanga wanaanzia hatua ya awali na Simba wameanzia hatua ya kwanza lakini wapotoshaji waliunda mijadala pori na wengine wakadanganya hadi kwenye mikutano ya waandishi wa Habari kuwa Yanga itaanzia hatua ya kwanza na Simba itaanzia hatua ya awali!

Ukweli umezima mijadala hiyo na hapa lilikuwa ni suala la muda tu ambalo limeweza kuipiga mijadala yote ya uongo na sasa wako kimya wakitunga mijadala mingine pori waianzishe kwa faida ya wanaowatuma kuipotosha jamii, jambo ambalo ni la hovyo sana katika maendeleo na mustakabari wa maendeleo ya mpira wetu.

Sasa Simba wamepangwa na Ahly, mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, timu kubwa zaidi kuliko zote barani Afrika na moja ya timu maarufu zaidi duniani.

Wanakwenda kucheza na Simba katika mechi mbili za kwanza kuwania kubeba ubingwa wa African Super League. Na kwa timu kama Ahly bila shaka watakuwa na nia kuu kutaka kuwa wa kwanza kulibeba kombe hilo jipya.

Simba wana mzigo mzito kweli, kweli wamekuwa wakifanya vema dhidi ya Ahly au timu nyingi za Afrika Kaskazini wanapocheza nazo kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, lakini sasa wanakutana na kigogo namba moja wa Afrika.

Si kazi nyepesi, haitakuwa lelemama na viongozi wa Simba lazima watakuwa wamejipanga na wanajua nini cha kufanya kwa kuwa hii si mara moja wanakutana na kigogo kama Ahly.

Mnaweza mkawaachia wakaendelea na kazi yao lakini mashabiki wanaweza kuwa nyenzo kubwa zaidi kuwaunga mkono kabla ya mechi na hata wakati wa mechi.

Kinachoweza kuwapa Simba nafasi ya kufanya vema ni kuhakikisha wanashinda Dar es Salaam na ikiwezekana ushindi mzuri. Mashabiki wanaweza kuwa nyenzo nzuri wakiungana na wachezaji wao kuwapa moyo, kuwahamisha, kuwaonyesha wako pamoja na watapambana pamoja dhidi ya vigogo hao wakubwa.

Kama sasa itakuwa ni lawama, kuwasema mitandaoni, kulalamika kwa kila jambo. Basi timu yao itaenda katika mechi dhidi ya Ahly ikiwa chini, ikiwa imechoka na inawezekana kukawa na ugumu sana.

Kuungana kutatengeneza umoja ambao unafanana na kauli mbiu ya Simba wenyewe, NGUVU MOJA. Na kutakuwa na wepesi wa kufanikiwa kumuangusha kigogo huyo Dar es Salaam na Simba itaendelea kuandika rekodi na kuiwakilisha Tanzania vizuri kama ilivyo sasa. Mkiamua, hili linawezekana.

Previous articleMWAMBA SKUDU AMPA NGUVU GAMONDI
Next articleAKUANZAE MMALIZE, ANGA LA BURUDANI LILIPATWA