MUZIKI unakua na muziki unatanuka na kupaisha mbawa zake kona mbalimbali za Dunia hii. Sio ajabu kumkuta mtu anasikiliza wimbo ambao hajui hata maana yake ila akaufurahia kwa hisia zake zote.
Katika muziki wa kufokafoka ‘Hip-Hop’ sio ajabu sana kukuta wasanii wakitupiana maneno au wakivimbiana kwa kitu fulani au jambo fulani. Huyu atasema yeye ni mkali na wengine watampinga kwa kudai wao ni bora kuliko yeye.
Kuna nyakati ni kama wasanii wachanga wanavunjika nyoyo zao kwa kuona wakubwa wao wakirushiana maneno. Hata hapa kwetu zimewahi zuka ‘beef’ zisizokuwa na maelezo ya kutosha kutokana na tofauti zao.
Wengine wakienda mbali zaidi kwa kusema hizi beef hasa za Bongo zinasukwa na media kwa manufaa yao wenyewe. Mambo kama hayo ya kurushiana maneno hayajawahi kuisha, yapo na yataendelea kuwepo.
Brian Ouko Omollo baada ya kuzaliwa Mama yake aliamua kumpa jina la Ouko kama kumuenzi mwanasiasa aliyeuwawa nchini Kenya, Hayati John Robert Ouko.
Brian Ouko ukipenda muite Khaligraph Jones aliibuka na kujimwambafai kuwa yeye ndiye rapper namba moja kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki. Hakuishia hapo tu aliongea na kuwapa ‘challenge’ wasanii wa Kibongo kumjibu kabla hajaivamia ‘industry’ ya HipHop Bongo na kuchukua kiti cha ufalme wa Rap nchini.
Khaligraph alianza harakati zake kati ya mwaka 2008, haikuwa safari ya kutoboa kiwepesi. Alipambana mpaka kuwa hapo alipo sasa. Kutoka katika shindano la ‘word and pictures’ akajulikana na baadae akashinda tuzo kutoka katika kituo kikubwa cha burudani kutoka bondeni kwa Madiba.
Jina lake likapaa alipotoa wimbo wa Mazishi ikiwa ni mwaka 2016 na hapo watu wakaanza kumpa masikio yao awaburudishe. Mwaka 2018 alifanikiwa kutoa albamu yake iliyokwenda kwa jina Testimony 1990, akaendelea na muziki akapokea tuzo mbalimbali.
Baada ya kipande chake cha video kusambaa katika mitandao ya kijamii akijinadi kuwa yeye ndiye mfalme wa muziki huo wa kufokafoka Afrika nzima, baadhi ya wasanii wakajitosa kutoa nyimbo za kumjibu kuwa yeye sio lolote wala sio chochote kwao.
Waswahili wanasema akuanzaye mmalize, naam! Hilo lilikamilishwa na wasanii wa muziki kutoka Tanzania kuamua kuingia ‘booth’ na kutema nyongo juu ya kile walichokiita kukosewa adabu na msanii huyo kutoka Kenya.
Baadhi ya wasanii ni kama Rosa Ree akiimba na kusema yeye ni MAMA OMOLLO, Chindo Man, Orbit, Young Killer, Songa, Motra the Future na wengine wengi waliachia nyimbo zao kwa kujibu mapigo mara baada ya kuachia ‘diss-track’ moja aliyoipa jina la BONGO FLAVOR. Hawakuwa nyuma walijibu mapigo bila kuonyesha unyonge wowote.
Wadau na wapenzi wa burudani ya muziki hawakusita kukaa kimya, kila mmoja akazungumza kwa namna alivyolipokea jambo hilo kutoka kwa msanii Khaligraph Jones. Wapo waliomjia juu na wengine kuona kama anatafuta kiki ili kuzungumziwa na watu.
Vituo mbalimbali vya burudani ndani na nje ya nchi walizungumzia kila hali ya vuguvugu hili lilivyokwenda huku baadhi ya wadau na wapenzi wa muziki wa kufokafoka wakitoa maoni yao ya moyoni juu ya kile kinachoendelea mitandaoni kati ya wasanii wa Tanzania na msanii kutoka Kenya, Khaligraph Jones ama ukipenda muite Papa Jones.
Wapo waliodai kuwa ni kiki, wengine wakaona ni kama Khaligraph anapoteza mashabiki zake nchini, wengine wakenda mbali na kudai kuwa ni nzuri sana kwani imeamsha muziki wa Hip Hop Afrika Mashariki, huku wakiongeza kuwa muziki huo ni kama ulilala na kuita kile alichoongea Jones kuwa ni kengele ya kuwaamsha kufanya muziki.
Kwake yeye anasema hakuna baya lolote alilokusudia, jambo lake kuu lilikuwa ni kuwaamsha wasanii kwani muziki wa Hip Hop ni kama ulikuwa umepoa kabisa ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Na aliyasema hayo alipojitokeza katika mitandao ya kijamii na kuongea kuwa hakuna swala la kuchukuliwa kwa uzito kwani hajawahi kuwa na tatizo na mtu na wala asichukuliwe vibaya.
Aliongeza zaidi kwa kusema anaambiwa kuna nyimbo nyingi hata za wasanii walikuwa hawafahamiki wakimtukana na hivyo amewapa nafasi ya kufanya wafahamike na kufatiliwa uwezo wao.
Ni kweli alikuwa na nia ya kuchangamsha ‘game’ ya muziki huu wa kufokafoka na vipi kama baadhi ya wasanii wakilibeba kama swala binafsi na kuchukulia kwa ukubwa wake?
Kwa chochote kile utakachokifanya katika maisha yako hakikisha umepima mbivu na mbichi, hakikisha umepima faida na hasara juu ya jambo unalotaka kwenda kulifanya.
Mpenzi msomaji, natumai nawe ulikuwa mmoja wa wafuatiliaji wa mambo hayo yaliyokuwa yakiendelea. Unaweza kuniandikia maoni yake juu ya faida na hasara ya kitu alichokifanya msanii huyo.