Home Sports MUDA WA YANGA KUREJESHA TABASAMU KWA WANANCHI

MUDA WA YANGA KUREJESHA TABASAMU KWA WANANCHI

WAKATI mwingine wa kuonyesha uimara kwenye mashindano makubwa kwa wawakilishi wa Tanzania Yanga.

Juni Mosi msafara wa Yanga uliwasili salama Algeria kwa kutumia ndege ya Air Tanzania ahadi iliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa imeshatimizwa.

Mchezo wa mwisho kwenye fainali dhidi ya USM Alger una picha ya tabasamu na maumivu kwa Watanzania kiujumla.

Kinachowezekana kwa sasa ni wachezaji wa Yanga kuonyesha utofauti kwenye mbinu na kupambana bila kuogopa kupata matokeo.

Muda wa kuamini kuhusu kuwa imara kwa matokeo ya ugenini umegota mwisho na ambacho kinatakiwa ni kila mmoja kupambana kwa ari kusaka ushindi.

Uzuri ni kwamba hakuna ambacho hakitawezekana ikiwa kutakuwa na nia ya dhati kwenye kutafuta matokeo.

Jambo la msingi ni kuamini kwamba ushindi upo ikiwa kila mmoja atajituma na kutimiza wajibu wake kwa wakati na umakini mkubwa.

Ushindi ugenini kwenye hatua ya fainali ni hatua kubwa na jambo ambalo linasubiriwa kwa shauku kubwa na kila mmoja kuona linatokea.

Wale ambao wamekata tamaa kwa muda huu ni muhimu kuamini kwamba mpira unadunda na dakika 90 zina matokeo ya kweli.

Kila mmoja anapenda kuona matokeo mazuri na hilo lipo kwa kila mmoja lakini wenye hatma ya timu kushinda ni wachezaji ambao watakuwa na uzi wa Yanga uwanjani.

Dakika 90 zitumike kwa kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na kurejea na taji kwenye ardhi ya Tanzania.

Muda wa kila Mtanzania kuiombea dua Yanga na ni muda wa wachezaji kujitoa kwa asilimia zote ndani ya uwanja bila kuogopa.

Previous articleSAA 8 ZA USO KWA USO, HERSI VS FEISAL
Next articleSIMBA WAANZA KAZI KUKAMILISHA MECHI MBILI