MATAJIRI WA DAR KWENYE DAKIKA 180 ZA MOTO

MATAJIRI wa Dar, Azam FC wanamechi mbili za moto kukamilisha mzunguko wa pili msimu wa 2022/23 kwa kucheza kete zao mbili.

Azam FC watacheza mchezo wa fainali Azam Sports Federation dhidi ya Yanga mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Yanga ilipata ushindi dhidi ya Singida Big Stars huku Azam FC ikiwatungua Simba, Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Awali mechi hizo mbili zilitarajiwa kuchezwa Mei 24 na 28 lakini kwa sasa zimepangiwa tarehe mpya na Bodi ya Ligi ya Mpira wa Miguu Tanzania, (TPLB).

Ni dhidi ya Coastal Union ya Tanga itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga hii itakuwa Juni 6 awali ilitarajiwa kuchezwa Mei 24 kete yao itakuwa dhidi ya Polisi Tanzania Juni 9 awali ilitarajiwa kuchezwa Mei 28.

Kwenye mechi hizo mbili moja watakuwa ugenini dhidi ya Coastal Union ambayo kwenye mzunguko wa kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 na kete ya pili watakuwa nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania ambao kwenye mzunguko wa kwanza walishinda bao 1-0 ugenini.

Ugumu upo kwenye mechi hizo kutokana na timu zote kusaka pointi tatu, Coastal Union inapiga hesabu za kulipa kisasi cha kufungwa ikiwa na pointi 33 nafasi ya 10 huku Polisi Tanzania ikipambana kutoshuka daraja ikiwa nafasi ya 15 pointi 25.

Kali Ongala kocha msaidizi wa Azam FC amesema kuwa wanatambua umuhimu wa mechi zilizobaki watafanya jitihada kupata pointi tatu.

“Tunatambua umuhimu wa mechi ambazo zimebaki tutafanya maandalizi muhimu kupata pointi tatu muhimu,” amesema.