SINGIDA BIG STARS YAIPIGIA HESABU YANGA

UONGOZI wa Singida Big Stars umeweka wazi kuwa upo tayari kwa mchezo wa hatua ya nusu fainali Azam Sports Federation dhidi ya Yanga.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Lite, Mei 21 na mshindi wa mchezo huo atatinga hatua ya fainali.

Ni Azam FC itakuwa inawatazama wababe hawa wawili kujua nani atacheza naye hatua ya fainali kwa kuwa wao walikata tiketi mapema walipomtungua Simba mabao 2-1 Uwanja wa Nangwanda, Sijaona.

Ofisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Masanza amesema kuwa maandalizi yapo vizuri na wanahitaji kupata ushindi.

“Tunatambua kwamba wapinzani wetu wapo imara na wanahitaji ushindi nasi tunafanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo huo ambao utakuwa mgumu.

“Wachezaji wapo tayari na benchi la ufundi linaendelea kuwapa mbinu wachezaji kwa ajili ya mchezo wa fainali, tunahitaji kupata matokeo chanya,”.

Miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye maandalizi ya mchezo huo ni pamoja na Pascal Wawa, Meddie Kagere,Bruno Gomes.