INGIZO jipya ndani ya kikosi cha Yanga, Clatous Chama ameliamsha balaa upya kutokana na mwendelezo wake wa ubora kwenye anga la kimataifa ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.
Chama amekuwa gumzo kwa kuwa kwenye mchezo dhidi ya Vital’O uliochezwa Uwanja wa Azam Complex waliposhinda mabao 6-0 Chama alikuwa kwenye ubora wake uleule alioufanya katika mchezo wa kwanza ambao nao ulichezwa Uwanja wa Azam Complex.
Ikumbukwe kwamba mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Agosti 17, Chama alifunga bao moja na kufikisha jumla ya mabao 19 katika Ligi ya Mabingwa Afrika nyota huyo ambaye aliibuka hapo akitokea Simba.
Kwenye mchezo wa Agosti 24 uliochezwa Uwanja wa Azam Complex aliweka rekodi ya kutoa hat trick ya asisti na kufunga bao bao moja kwenye mabao sita ambayo yalifungwa na Yanga huku akitimiza pasi nne na bao moja linamfanya afikishe jumla ya mabao 20 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Usajili wake ulileta gumzo akiwa ni mchezaji wa kwanza kutambulishwa ndani ya Yanga ilikuwa ni Julai Mosi 2024 ambapo inatajwa kwamba Simba bado walikuwa wanahitaji saini yake ila mwamba huyo alichagua kupata changamoto mpya kwa watani zao wa jadi ambapo aliwashukuru Simba kwa muda aliokuwa hapo.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga aliweka wazi kuwa miongoni mwa wachezaji wenye ubora mkubwa na uwezo uwanjani ni pamoja na Chama hivyo anaungana na wachezaji wengine bora katika kutimiza majukumu ndani ya uwanja.
“Chama ni yuleyule na amepewa jezi ileile aliyokuwa anavaa alipokuwa kule ili wasimsahau wakimuona kwa kuwa ni mchezaji ambaye anajulikana na ni mkubwa yupo kwenye timu kubwa.”
Yanga imevuka hatua ya awali kwa ushindi wa jumla ya mabao 10-0 ambapo ndani ya dakika 180 timu hiyo haijaruhusu bao la kufungwa ndani ya uwanja kwenye anga la kimataifa.