Home Uncategorized KIUNGO SIMBA AWATAKA RAJA CASABLANCA

KIUNGO SIMBA AWATAKA RAJA CASABLANCA

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mmalawi Peter Banda amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo, kwa kuwaambia kuwa amepona na yupo fiti kucheza mchezo wa mwisho wa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itavaana dhidi ya Raja Casablanca saa 7:00 usiku wa kuamkia Jumamosi huko nchini Morocco katika mchezo wa marudiano unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.

Katika mchezo huo, Simba itaingia uwanjani kuvaana na Raja Casablanca wakiwa na hasira za kutoka kufungwa mabao 3-0 walipocheza kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Kiungo huyo alipata maumivu ya misuli katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Afcon walipovaana dhidi ya Misri.

Akizungumza na Championi Jumatano, Banda alisema kuwa hakupata majeraha makubwa akiwa katika majukumu ya timu ya Taifa ya Malawi kiasi cha kumfanya aukose mchezo dhidi ya Raja Casablanca.

Banda alisema kuwa, alishindwa kuendelea na mchezo huo na kutolewa nje kutokana na maumivu madogo aliyoyasikia kabla ya kuomba atolewe nje kwa manufaa ya timu yake.

Aliongeza kuwa anashukuru hivi sasa anaendelea vizuri na yupo fiti kuipambania timu yake ya Simba itakapokwenda kulipa kisasi cha kufungwa dhidi ya Raja Casablanca.

“Sikupata majeraha yoyote mwilini kwangu zaidi ya maumivu pekee niliyoyasikia ambayo niliyapata dakika ya 60 ya mchezo na kuomba nitolewe nje kwa hofu ya kuumia zaidi.

“Hivyo Wanasimba wasiogopeshwe kwa mimi kutolewa kwa machera na kushindwa kuendelea kucheza mchezo dhidi ya Misri, kwani nipo vizuri hivi sasa.

“Niliumia, haikuwa jeraha kubwa ni maumivu madogo tu, nitakuwa fiti kwenye mchezo ujao dhidi ya Raja Casablanca,” alisema Banda.

Previous articleMBRAZIL APITISHA PANGA KIMYA KIMYA SIMBA
Next articleCONTE KASEPA NA KAKA YAKE SPURS