Home Sports SIMBA KUMSHUSHA MSHAMBULIAJI HUYU WA KAZI

SIMBA KUMSHUSHA MSHAMBULIAJI HUYU WA KAZI

IMEELEZWA kuwa Sh 800Mil alizoweka Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ kwa ajili ya usajili, zimeanza na mshambuliaji wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Kwame Peprah, raia wa Ghana.

Simba imekuwa kwenye mazungumzo ya muda mrefu na Mghana huyo ambaye inaelezwa mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Timu hiyo imepanga kukiimarisha kikosi chao katika msimu ujao baada ya huu kuonekana kutokuwa na timu imara na bora na kusababisha kupoteza makombe yote waliyokuwa wakiyatetea – Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).

Taarifa zimeeleza kupitia kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, tayari Kwame yupo nchini na amefichwa kwenye moja ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa mabosi wa Simba hivi sasa, wanafanya taratibu za kukamilisha uhamisho wake huku ishu hiyo ikiwa chini ya Mo, Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa zamani wa timu hiyo, Crescentius Magori na Muramu Ng’ambi.

“Naomba nikuhakikishie tu kuwa msimu huu tumejipanga kusuka kikosi cha kimataifa kweli, na kwa kukudhihirishia hilo, tayari tumeshaanza harakati za usajili na muda huu tunaozungumza yule straika wa Orlando Pirates, Mghana Peprah tayari yupo kwa ajili ya kukamilisha usajili wake, yupo katika moja ya hoteli, tofauti na mshambuliaji huyo, wapo wachezaji wengine wapya wa kigeni tutakaowasajili wa kiwango cha juu.

“Kwa kifupi ni kwamba usajili wetu msimu huu si wa kitoto kwani upo chini ya watu sahihi kwa maana ya Mo, Magori na Muramu, wameamua kuweka kikundi chao maalum ili kuhakikisha wanafanikisha kupata wachezaji watakaotufikisha kwenye malengo yetu katika michuano ya kimataifa mwakani, hivyo kuna wachezaji watano wa kimataifa watatua msimu huu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alipotafutwa alisema: “Usajili wetu tumepanga kuufanya kimyakimya na utajulikana mara baada ya kumalizana na mchezaji husika.”

Chanzo:Championi

Previous articleUWANJA WA AMAAN:TANZANIA 0-0 CAMEROON
Next articleTANZANIA YAFUNZU KOMBE LA DUNIA