Home Sports YANGA KUINGIA KAZINI KWA MARA NYINGINE TENA

YANGA KUINGIA KAZINI KWA MARA NYINGINE TENA

KIKOSI cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu,Nasreddine Nabi kesho Mei 4 kinatarajiwa kushuka uwanjani kusaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting.

Tayari kikosi hicho kimewasili salama Kigoma na kupokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki ambao walijitokeza jana Mei 2.

Ni mchezo wa mzunguko wa pili baada ya ule wa kwanza Yanga kushinda mabao 3-1 Uwanja wa Mkapa na Ruvu wao walipoteza pointi tatu.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa mapokezi ambayo wameyapokea yanawapa tabasamu kubwa wachezaji pamoja na viongozi.

“Ni furaha kwetu na wachezaji kwa namna ambavyo tumepokelewa hivyo tuna amini kwamba mchezo wetu utakuwa mzuri na tunahitaji kupata ushindi.

“Tunajua kwamba mchezo utakuwa mgumu nasi tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa,” amesema Bumbuli.

Yanga ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 55 inakutana na Ruvu Shooting iliyo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 21.

Jana walifanya mazoezi wachezaji ikiwa ni pamoja na Feisal Salum, Djuma Shaban,Said Ntibanzokiza, Fiston Mayele.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 10:00 jioni Uwanja wa Lake Tanganyika.

Previous articleSIMBA KUIKABILI NAMUNGO WAKIWA NA HOFU
Next articleNAMNA YANGA NA SIMBA WALIYVOWAPA MKWANJA TFF