Home Sports MASTAA YANGA WAKOMBA MABILIONI YA BONASI

MASTAA YANGA WAKOMBA MABILIONI YA BONASI

USHINDI wa 11 walioupata Yanga, umewapa wachezaji wa timu hiyo bonasi ya Sh 265Mil katika michezo ya Ligi Kuu Bara tangu kuanza kwa msimu huu. Hiyo ikiwa ni siku chache tangu watoke kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, mchezo uliopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.


Ushindi huo umewafanya waendelee
kukaa kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 35 wakicheza michezo 13 ya
ligi, huku watani wao Simba wakifuatia
wakivuna pointi 25 wakibakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Yanga tangu kuanza kwa msimu huu, wameshinda michezo 11 huku wakitoka suluhu miwili dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar nyingine na Namungo FC nayo ilichezwa Uwanja wa Ilulu, Lindi.

Ipo hivi, wadhamini wa Yanga ambao ni GSM mara baada ya kuanza kwa msimu waliwaahidi wachezaji kuwapa Sh 20Mil katika katika kila ushindi wa mchezo wa ligi.

Lakini katika michezo miwili ambayo ilikuwa migumu dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga matajiri hao waliongezewa bonasi na kufikia sh 35Mil kama wakiwafunga, ikaja kuongeza na kufikia Sh 50Mil walipowavaa Polisi Tanzania ambayo yote walifanikiwa kushinda na kuchukua Sh 85Mil.

Mastaa hao wakishinda michezo hiyo 11 ya ligi walijikuta wakichukua Sh 265Mil zilizogawiwa kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo, linaloongozwa na Kocha Mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi.

Hivyo wachezaji hao katika michezo 11 waliyocheza na kushinda, tisa walivuna Sh 180Mil kutokana na bonasi ya Sh 20Mil kabla ya kuongezewa dhidi ya Coastal na Polisi Tanzania ambazo zilifikia Sh 265Mil. Wadhamini hao, huenda wakaendelea kutoa bonasi ya Sh 50Mil katika michezo miwili ya mwisho ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi watapocheza dhidi ya Mbeya City na Geita Gold.


Wachezaji hao
wameahidiwa kupewa bonasi ya ushindi pekee, kama wakitoa sare hakutakuwa na bonasi, umewekwa utaratibu huo kwa ajili ya kuongeza hamasa ya wachezaji kupambana kupata ushindi pekee utakaowafanya
watwae ubingwa mwishoni
mwa msimu.


Mkurugenzi Uwekezaji wa
GSM ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said,
hivi karibuni alizungumzia
hilo la bonasi na kusema kuwa: “Bonasi ipo kwa wachezaji wetu ambayo
maalum kwa ajili ya
kuongeza hamasa wakiwa uwanjani.


“Bonasi hiyo imekuwa
ikibadilika kwa kuongezeka kutokana na aina ya timu tunayokutana nayo. Na bonasi ni siri kati ya uongozi na wachezaji.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Previous articleYANGA WATUA MWANZA KIBABE, KUWAVAA MBAO JUMAMOSI
Next articleYANGA WAMEPANIA, GSM WAMUITA MAYELE