Home Sports SIMBA YACHEZA DAKIKA 180 BILA KUFUNGA

SIMBA YACHEZA DAKIKA 180 BILA KUFUNGA

PABLO Franco ana kazi kubwa ya kufanya kwa sasa ndani ya Simba hasa kwenye safu ya ushambuliaji ambayo imeweza kuyeyusha dakika 180  bila kufunga.

Ile safu yenye mshambuliaji bora msimu wa 2020/22 John Bocco ambaye alifunga mabao 16 na pasi mbili mpaka sasa bado inapitia wakati mgumu.

Ilianza kunyooshwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City ambapo hapo washambuliaji wote walicheza ikiwa ni Chris Mugalu, Meddie Kagere, Kibu Dennis na Bocco.

Washambuliaji hao wamekuwa na vigugumizi kwenye miguu kwa kuwa walikosa nafasi za wazi zaidi ya tatu ikiwa ni pamoja na penalti iliyokoswa na Chris Mugalu dakika ya 48 na Bocco pia shuti lake liliokolewa na kipa Deogratius Munish.

Mchezo wa pili ilikuwa mbele ya Mtibwa Sugar ambapo walikamilisha dakika 180 bila kufunga na hapo muziki wote ulikuwa uwanjani ikiwa ni pamoja na ingizo jipya Clatous Chama ambaye aliyeyusha dakika 45.

Kwenye mechi 12 imefunga mabao 14 na kinara wa mabao ni Meddie Kagere mwenye mabao manne na pasi moja ya bao kituo kinachofuata ni Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kushindwa kufunga ndani ya dakika 180 ni jambo ambalo ni baya kwao.

“Simba kushindwa kufunga ndani ya dakika 180 ni jambo baya hasa ukizingatia kwamba kuna wachezaji kama Chris Mugalu, John Bocco na Meddie Kagere,”.

Kituo kinachofuata ni dhidi ya Kagera Sugar mchezo unaoatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Kaitaba, Januari 26.

Previous articleCOMOROS KUVAANA NA CAMEROON YENYE KINARA WA UTUPIAJI
Next articleGABON WAMEPENYA AFCON NA KUTINGA ROBO FAINALI