JEMBE JIPYA SIMBA KUANZA NA MTIBWA SUGAR MANUNGU

JANUARI 22,2022 leo mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Mtibwa Sugar na Simba unatarajiwa kuchezwa saa 10:00 jioni ambapo mashabiki wa Simba wameambiwa wasubiri kuona kikosi kamili.

Miongoni mwa nyota ambao wanatarajiwa kuanza leo ni pamoja na Clatous Chama ambaye ni ingizo jipya kwa mara nyingine tena ndani ya kikosi cha Simba.

Chama amerejea Simba akitokea kikosi cha RS Berkane ambapo alijiunga nacho msimu huu mwanzoni akitokea kikosi cha Simba lakini amerejeshwa tena ndani ya Simba kuendelea palepae alipoishia.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2020/21 akiwa na Simba aliweza kufunga mabao nane na alitoa pasi 15 za mabao na kumfanya awe ni namba moja kwenye kutengeneza pasi za mwisho.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameweka wazi kwamba masuala ya vibali kwa Chama yamekamilika na anaweza kuanza mbele ya Mtibwa Sugar.

“Kuhusu vibali vya mchezaji Chama tayari vimekamilika hivyo mashabiki watarajie kumuone leo Uwanja wa Manungu akitimiza majukumu yake.

“Mchezo utakuwa mgumu hasa ukizingatia kwamba tumetoka kupoteza mchezo wetu uliopita tutapambana kufanya vizuri,” amesema.

Mtibwa Sugar mchezo wao uliopita walilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting na Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.