USAJILI UMEKWISHA SASA KAZI IENDELEE

    USHINDANI  kwenye ligi unazidi kushika kasi kila iitwapo leo hilo ni jambo jema kwa kuwa ili ligi iwe bora na imara ni muhimu ushindani uwepo.

    Pia tumetoka kumaliza suala la masuala ya usajili hasa ilikuwa ni dirisha dongo ambalo lilikuwa ni maalumu kwa ajili ya maboresho kwenye timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, Championship, Ligi ya Wanawake.

    Ilikuwa namna hiyo kwa wale ambao walikuwa wanahitaji kufanya hivyo wamekamilisha hesabu zao na kuna timu nyingine ziliweka wazi kwamba hazina mpango wa kuongeza nguvu kwa kuwa wanajitosheleza hilo nalo ni sawa.

    Ushindani mkubwa ambao upo ni mzuri na inabidi uendelee kwa kuwa kuna jambo zuri linakuja hapo baadaye kwenye ligi zetu.

    Hali hii inaleta picha nzuri kule ambako tunatarajia kwenda kutokana na kila mmoja kuwa na kitu ambacho anakifikiria kwa sasa na anakitenda kwa wakati.

    Wale ambao wapo Ligi Championship wanajua kile namna ushindani ulivyo mkubwa na kila timu inavyopambana kusaka ushindi kwenye mechi zake.

    Hamna namna ya kufanya kwa sasa kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kwa kuwa kwenye ushindani ni lazima aonekane ambaye anashindwa.

    Zipo ambazo zimekuwa zikishindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao ambazo zimepita hilo ni muhimu kulifanyia kazi wakati huu baada ya kukamilisha maboresho.

    Kwa wachezaji ambao wamepata timu mpya kwa wakati huu na wale ambao wameongeza mikataba yao basi wajue kwamba kazi yao ni moja kucheza mpira.

    Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.

    Ila imekuwa bahati mbaya kila wakati timu nyingi kuanza kuonyesha ushindani kwenye mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama jambo ambalo huwaongezea ugumu kufanya vizuri.

    Ushindani na ule mchezo wa kusaka pointi tatu ni muhimu uwe unaonekana kwenye kila mechi bila kujali ni timu ipi ipo nafasi ipi.

    Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.

    Wachezaji wakiweza kufanya yale ambayo wanaelekezwa na benchi la ufundi inakuwa ni rahisi kwao kupata ushindi pia jitihada binafsi zinahitajika kwa wachezaji katika kusaka matokeo.

     Zipo timu ambazo ziliwahi kupanda daraja  zilianza vizuri mwanzo lakini zilipokuja kukwama kusaka matokeo ziliweza kurejea zilikokuwa zimetoka hili nalo liwe ni somo kwa timu zote.

    Matumaini yangu ni kwamba kupitia matukio haya yanayoendelea wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.

    Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.

    Kwa upande wa Ligi ya Wanawake huku tunaona kwamba mambo yanazidi kuendelea kwa timu kusaka ushindi basi iwe hivyo bila kuchoka.

    Pongezi nyingi kwa makocha namna ambavyo wanawapa mbinu wachezaji wao ili waweze kwenda sawa na hali ya ushindani ambayo ipo.

    Zawadi kubwa huku iwe kwenye kuwaboreshea mazingira yao ya kazi hasa kuanzia viwanja pamoja na vitendea kazi.

    Katika hili pia iwe fundisho katika kuangalia usalama na uwepo wa wachezaji wetu kwani wanajitoa kwa ajili ya kazi hivyo nao pia wapewe kipaumbele.

    Kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama namna ya kuwapiga tafu zaidi ya wakati huu kwa wachezaji pamoja na timu kiujumla kwani wengi hali zao bado hazijawa kwenye usawa hasa katika masuala ya maandalizi pamoja na fedha.

    Mazingira magumu ya maandalizi yanafanya timu iweze kufungwa mabao mengi kwenye mchezo mmoja hili jambo sio nzuri kwani tunahitaji kuona ushindani wa kweli.

    Katika hili ni muhimu kutazama namna maandalizi yalivyo pamoja na fedha ambazo zinatumika kwenye maandalizi kamili kwa timu.

    Timu chache zina uhakika kuhusu posho na stahiki za wachezaji na hii ni mbaya kwani mambo yakiwa hivi ushindani utazidi kupungua kwa wale ambao mambo yao ni magumu.

    Previous articleYANGA:TUNA KIKOSI IMARA CHA KAZI,YAFUNGUKIA ISHU YA CHAMA
    Next articleHATUA YA MAKUNDI YA AFCON INATAMATIKA, EPL, EFL CUP NAKO MAMBO SAFI!