KIUNGO Mnigeria, Udoh Etop David, amethibitisha kwamba, hajafanikiwa kupata mkataba wa kuitumikia Simba baada ya kufanya majaribio kwa takribani wiki moja.
Udoh akiwa kwenye majaribio hayo, alifanikiwa kucheza mechi mbili za Kombe la Mapinduzi, lakini ameshindwa kumshawishi Kocha Pablo Franco.
kiungo huyo mkabaji, amesema licha ya kutarajia kupewa mkataba na timu hiyo, lakini hajafanikiwa na kwa sasa kitu ambacho anatarajia ni mipango ya safari yake kutoka Tanzania kurudi kwao Nigeria.
“Maisha ya Tanzania ni mazuri na nimeyapenda sana, ndani ya Simba nimekaa vizuri kuanzia kambini hadi kwenye mechi.
“Kuhusu kupewa mkataba na Simba hapana,hakuna maisha mengine tena ndani ya Simba.
“Kwa sasa naangalia mipango yangu ya kuondoka Tanzania kurudi nyumbani Nigeria,” amesema.
Kwenye Kombe la Mapinduzi nyota huyo alikwama kufunga bao wala kutoa pasi ya bao na alishuhudia timu hiyo ikisepa na Kombe la Mapinduzi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.