UKISIKIA watu wanakwambia Simba wamefanya kufuru, basi amini kwamba ufanikishaji wa kuipata saini ya kiungo Mzambia, Clatous Chama imetumika gharama kubwa sana.
Chama ambaye amerejea Simba na kusaini mkataba wa miaka miwili, aliondoka kikosini hapo Agosti 2021, baada ya kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo kuanzia msimu wa 2018/19 hadi 2020/21 na kutua RS Berkane ya Morocco.
Pia Chama alikuwepo kwenye kikosi cha Simba kilichocheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili msimu wa 2018/19 na 2020/21.
Kiungo huyo baada ya kutua RS Berkane, amefanikiwa kukaa huko kwa takribani miezi mitano kabla ya kurudi Simba.
Chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, dau la usajili wa Chama limegharimu dola 150,000 (sawa na Sh 344,697,000 za Kitanzania).
Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, mshahara wake kwa mwezi ni dola 15,000 (sawa na Sh 34,469,700 za Kitanzania) ambapo ndani ya miaka miwili ikiwa na jumla ya miezi 24, atalipwa Sh 827,272,800 za Kitanzania.