MSUVA APANDIWA DAU NA YANGA ,SIMBA

WAKATI dirisha dogo la usajili hapa nchini likifungwa usiku wa kuamkia leo Jumapili, kulikuwa na mchuano mkali kwa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya kupata saini ya kiungo mshambuliaji wa Wydad Casablanca ya Morocco, Mtanzania, Simon Msuva.

Msuva aliondoka Yanga, Julai 29, 2017, akiwa ameisaidia kuvuna mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara na kutua Difaa El Jadida ya Morocco, kisha Novemba 10, 2020, akajiunga na Wydad.

Habari zimeeleza kwamba, mabosi wa timu hizo, kila mmoja kwa wakati wake alifanya mazungumzo na Msuva kuona dili linakamilika.

Kwa upande wa Simba, inaelezwa kwamba, katika majadiliano yao, Msuva aliomba kupatiwa dau la usajili dola 100,000 (sawa na Sh 229,798,000 za Kitanzania) na mshahara dola 10,000 kwa mwezi (sawa na Sh 22,979,800 za
Kitanzania).

“Sisi kama Simba tumepambana sana kuipata saini ya Msuva, maana tuliamini kabisa endapo akija kwetu tutakuwa na kikosi cha ushindani sana.

“Katika majadiliano ya kumsajili, aliomba apatiwe dola laki moja na mshahara wa dola elfu kumi, akikubali kusaini
mkataba wa mwaka mmoja.

“Yanga nao tunasikia walikuwa wakimfukuzi, hivyo kulikuwa na vita kubwa ya kuona nani atafanikiwa kukamilisha usajili wake,” kilisema chanzo hicho.

Spoti Xtra lilimtafuta Msuva kuzungumzia ishu hiyo ambapo alisema: “Hadi muda huu hakuna suala jipya, isipokuwa vuta subira ili yakiwa poa, nitakupa habari utoe rasmi.”