>

MAYELE ATUMA UJUMBE HUU COASTAL UNION

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele, amesema kuwa kwa sasa malengo yao yote ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo wao unaofuata wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union.

Yanga kesho Jumapili wanatarajiwa kumenyana na Coastal Union wakiwa ugenini katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa ligi kuu waliocheza katika uwanja huo msimu uliopita ambapo walipoteza kwa kufungwa 2-1.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mayele alisema kuwa baada ya kufanya vibaya katika michuano ya Mapinduzi sasa akili zao zote ni katika kuhakikisha kuwa wanapata ushindi katika mchezo wao unaofuata wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union.

“Malengo yetu siku zote ni kushinda kila mechi, tumetoka kufanya vibaya katika Mapinduzi mara baada ya kuwa nje ya malengo, hivyo lazima tupambane tuweze kushinda mchezo uliopo mbele yetu ili kuwapa furaha mashabiki wetu ambao wameumia na kilichotokea.

“Najua mchezo utakuwa mgumu kutokana na timu nyingi kuhitaji kupata matokeo wanapokutana na Yanga lakini kwa kuwa na sisi tunalitambua hilo, lazima tuhakikishe tunapata kile kilicho bora dhidi yao,” alisema mshambuliaji huyo.