MOHAMED Salah amesema hatma yake ndani ya Liverpool iko mikononi mwaka bodi ya klabu hiyo, ila yeye anapenda kuendelea kubaki Anfield.
Ishu ya Salah kusaini mkataba mpya ndani ya Liverpool imekuwa ikizungumzwa tangu mwaka jana lakini hakuna muafaka uliofikiwa mpaka sasa.
Salah anatarajiwa kumaliza mkataba wake ndani ya miezi 18 ijayo katika klabu hiyo na yeye anatamani kustaafia soka lake hapo.
Staa huyo alitua Liverpool mwaka 2017 akitokea Roma kwa pauni 34m.
Inaelezwa kuwa katika mkataba wake mpya nyota huyo anadaiwa kuhitaji kiasi cha mshahara wa pauni 350,000 kwa wiki na atakuwa mchezaji ambaye analipwa vizuri kwa muda wote ndani ya Liverpool. Salah amesema: “Nataka kubaki hapa, ila maamuzi hayapo mikononi mwangu. Wanafahamu ninachotaka sijaomba vitu vya kutisha nimeomba kile kitu ambacho wana uwezo nacho na sio vinginevyo.
“Nimekuwa hapa kwa msimu wa tano sasa, naifahamu klabu yangu vizuri, nawapenda mashabiki, lakini uongozi wao unajua hali halisi na wao ndiyo watafanya maamuzi.”