JAMAA HAWA WANA MIBALAA WATAKIWASHA KOMBE LA MAPINDUZI

MADOAMADOA yote yaliyojificha yatajulikana leo kutokana na balaa ambalo limejificha kwa nyota hawa ambao wanapewa nafasi ya kuweza kukinukisha katika fainaliya Kombe la Mapinduzi.

Hapa Spoti Xtra inakuletea nyota wa Simba na Azam FC ambao wanatarajiwa kusaka mbabe atakayesepa na taji lililokuwa linatetewa na Yanga namna hii:-

Aishi Manula

Kipa namba moja wa Simba anapewa nafasi ya kuweza kuanza langoni leo kutokana na mwendo wake kuwa bora ndani ya Kombe la Mapinduzi.

Simba ikiwa imecheza mechi tatu yeye ameanza langoni kwenye mechi mbili ambazo ni dakika 180 ilikuwa mbele ya Mlandege na Namungo FC na kwenye mechi zote hizo hakuweza kutunguliwa.

Anakumbukwa namna alivyoweza kuonyesha balaa katika kuokoa hatari mbele ya Namungo FC ilikuwa ni dakika ya 42,56,60,74 na 88 na kulifanya lango lake kuwa salama mbele ya Obrey Chirwa na Shiza Kichuya ambao walikuwa wakiliandama lango lake.

Rally Bwalya

Hana baya hasa kwenye mguu wake wa kushoto hapo ndipo balaa lake limejificha. Amecheza mechi mbili ilikuwa mbele ya Selem View na alipachika bao moja kwa mguu wake wa kushoto akiwa nje ya 18 na ule wa pili ilikuwa dhidi ya Namungo FC.

Meddie Kagere

Mzee wa kukaa kwenye nafasi hasa pale anapokuwa na viungo wa kumtengeneza mabao, aliweza kufunga bao mbele ya Namungo FC na kuongeza nguvu kwa Simba kutinga hatua ya fainali.

Pape Sakho

Nyota ambaye amekuwa na hatari kila awapo uwanjani kwa sasa kwenye Kombe la Mapinduzi na amefunga mabao mawili akiwa ni kinara wa utupiaji kwa upande wa Simba. Mbele ya Selem View na Namungo aliweza kufunga hivyo ana balaa kwenye kila mechi ambazo ameanza alifunga.

Henock Inonga

Beki wa kazi chafu, hana maswali mara mbilimbili kwenye kuanua majalo yanapofika miguuni mwake, spidi ya kupanda na kushuka ni balaa lake na ni mwepesi kukasirika.

Jonas Mkude

Mmiliki wa eneo la kati, kazi chafu zinatengenezwa kwake.Kakinukisha kwenye mechi zote tatu akianza kikosi cha kwanza na hajashuhudia timu yake ikifungwa.

Sadio Kanoute

Kukiwa na migongano mingi huwezi kumuona Kanoute labda ataibukia kwenye kona kwa kuwa ni mtu wa kugusa na kuachia.

Kibu Dennis

Ni chaguo namba moja la Kocha Mkuu, Pablo Franco na amekuwa akiwapa tabu mabeki wa timu pinzani pale wanapokutana.

Azam FC

Frank Domayo

Moja ya nyota wa kazi chafu ndani ya Azam FC balaa lake muda wote tu. Ikumbukwe kwamba Julai Mosi 2020 kwenye mchezo wa robo fainali wa Kombe FA wakati Simba ikishinda mabao 2-0, Domayo alimchezea faulo mbaya Shomari Kapombe.

Pia alionyesha balaa kwenye mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Mapinduzi mbele ya Zawad Mauya ambapo alimchezea faulo mbaya, Zawad Mauya dakika ya 69 hivyo ni nyota mwenye balaa kila aanzapo uwanjani.

Daniel Amoah

Hana mambo mengi yeye anapiga kazi tu anapanda na kushuka kibindoni ana bao moja  na alitumia vema pasi ya mshikaji wake Edward Manyama.

Tepsi Evance

Lile balaa aliloonyesha mbele ya Yanga kwenye hatua ya nusu fainali kwa mabeki halikuwa la kitoto na alifanya yake, pia hata Simba walipokutana nao kwenye mchezo wa ligi wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 2-1 Azam FC pasi ya bao ilitoka kwenye mguu wa Tepsi.

Ibrahim Ajibu

Jamaa huyu ni mzee wa kujibu majibu ya wana Azam FC kwa sasa akiwa anapewa nafasi ya kuweza kuanza mbele ya mabosi wake wa zamani.

Alipokutana na mabosi wake wa zamani Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi alipewa jukumu la kupiga faulo na alicheza faulo tatu na kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 67 balaa lake sio dogo.

Edward Manyama

Kinara wa pasi za mwisho ndani ya Azam FC kwenye Kombe la Mapinduzi akiwa nazo mbili kati ya mabao 7. Kazi ya mipira iliyokufa itakuwa kwenye miguu yake katika kuonyesha balaa.

Idris Mbombo

Ingizo jipya ndani ya Azam FC linakwenda kupambana na mshikaji wake Inonga ambaye naye ni raia wa Congo, balaa lao huwa kubwa na ametupia mabao mawili.

Agrey Morris

Kisiki wa kazi ukuta wake mpaka sasa umeruhusu kufungwa bao moja kwenye mechi nne ambazo Azam FC imecheza.

Mathias Kigonya

Hakuwa na bahati ya kuokoa penalti mbele ya Yanga kwa kuwa Yassin Mustapha alipaisha lakini umbo lake la miraba minne likiwa langoni linatisha.