MOTO WA KIBU DENNIS HAUPOI

MOJA ya washambuliaji ambao wameweza kuandika rekodi ya kipekee kwa msimu wa 2021/22 ndani ya Simba ni pamoja na Kibu Dennis ambaye alipopata nafasi ya kufunga bao la kwanza moto wake haujazima.

Baada ya kufanikiwa kupachika bao hilo kwenye kila mchezo ambao amecheza ndani ya ligi katika mechi nne mfululizo ambazo ni dakika 360 amekuwa ni sehemu ya ushindi wa timu hiyo.

Kasi yake ipo hivi

Novemba 19 2021 mbele ya Ruvu Shooting, Uwanja wa CCM Kirumba aliweza kufunga bao lake la kwanza kwenye ligi akiwa na uzi wa Simba baada ya kuibuka hapo akitokea Klabu ya Mbeya City ilikuwa dakika ya 44 kwa mguu wake wa kushoto akiwa ndani ya 18 kwa pasi ya mshikaji wake Meddie Kagere.

Desemba Mosi 2021 aliweza kutoa pasi yake ya kwanza kwenye ligi akiwa na Simba mbele ya Geita Gold ilikuwa Uwanja wa Mkapa na alimpa mshikaji wake Peter Banda dakika ya 9 kwa mguu wake wa kulia akiwa ndani ya 18.

Desemba 24 alikuwa nyota wa mchezo mbele ya KMC wakati wakishinda mabao 4-1 kwa kuwa aliweza kutupia jumla ya mabao mawili mwenyewe katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Alitupia mabao hayo dakika ya 46 akiwa ndani ya 18 na 57 ambapo hili alitupia akiwa nje ya 18 na kufanya aweze kufikisha jumla ya mabao matatu kwenye ligi na yote alitumia mguu wa kushoto.

Pia Januari Mosi 2022 aliweza kufungua mwaka kwa kutoa pasi yake ya pili ambapo alimpa mshikaji wake Pape Sakho ilikuwa mbele ya Azam FC mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa na alitoa pasi hiyo akiwa nje ya 18 kwa mguu wake wa kulia.

Mguu aupendao

Kwenye mabao hayo matano ambayo amehusika ndani ya Simba ni mabao matatu ametumia mguu wa kushoto na mabao mawili mguso wake ulikuwa ni kwa mguu wa kulia.

Mechi zake

Alitumia dakika 45 mbele ya Tanzania Prisons,dakika 90 mbele ya Coastal Union,dakika 90 mbele ya Namungo, dakika 90 mbele ya Ruvu Shooting,dakika 88 mbele ya Geita Gold,Yanga dakika 90, KMC dakika 82 na mbele ya Azam FC alitumia dakika 90.

Jumla ameyeyusha dakika 637 kwenye mechi 9 kati ya 10 ambazo Simba imecheza alikosekana kwenye mchezo mmoja ilikuwa dhidi ya Biashara United.

Maneno ya makocha waliomfundisha

Kocha wa zamani wa Simba, Didier Gomes aliliambia Championi Jumatatu kuwa Kibu ni mchezaji mwenye uwezi mkubwa lakini anapaswa kujiamini.

“Kibu kuna kitu ambacho anacho ni moja ya washambuliaji wazuri anahitaji muda kufanya vizuri zaidi kwani kuna kitu ambacho anacho,”.

Kim Poulsen, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania amesema kuwa anaamini kwamba Kibu akiendelea kujituma atakuja kuwa bora.

“Nilikuwa na Kibu kwenye timu ya taifa na ninaona kwamba kuna timu ambazo zilimuona kupitia kwenye mechi alizocheza, kukosa kwake nafasi ni jambo ambalo lipo lakini ninaona kwamba anazidi kuimarika,”.

Pablo Franco, Kocha Mkuu wa Simba kwa sasa amesema kuwa kuna mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi hasa kwenye umaliziaji wa nafasi zinazotengenezwa.

“Kila mchezaji anatimiza majukumu yake na nina amini kwamba maboresho yanahitajika kwenye upande wa umaliziaji,” amesema.