KUELEKEA mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi rasmi kesho Jumanne, uongozi wa Simba umetamba kuwa kikosi chao kiko tayari kwa ajili ya mashindano hayo na malengo yao makubwa ni kuwavua ubingwa watani zao wa jadi Yanga.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi ilianza rasmi jana Jumapili kwa mchezo mmoja kati ya Namungo dhidi ya Meli 4 City. Kuelekea michuano hiyo Simba leo inatarajiwa kusafiri kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano hiyo, ambapo msimu uliopita walicheza hatua ya fainali.
Simba juzi Jumamosi katika Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam walikuwa wenyeji wa Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, ushindi ambao umeifanya Simba kufikisha pointi 24 katika michezo 10 waliyocheza mpaka sasa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema: “Tunajivunia mwenendo ambao kikosi chetu umekuwa nao kwa sasa, baada ya kumaliza mchezo wetu uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Azam mipango yote ni kuelekea michuano ya Kombe la Mapinduzi.
“Tutakwenda kwenye michuano hii tukiwa na ari na mipango ya kuhakikisha tunaibuka mabingwa, lakini pia hii itakuwa sehemu ya kikosi chetu kupata mazoezi ya ziada kwa ajili ya kuongeza muunganiko wa timu
hususani kwa nyota wapya ambao watajiunga na kikosi chetu kwenye dirisha hili la usajili.”